Kilimanjaro. Mkurugenzi Msaidizi wa Usimamizi wa Mashirika Yasiyo ya Kibiashara kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw. Joseph Mwaisemba, amefanya ziara ya kikazi katika Shamba la Miti West Kilimanjaro na kutoa pongezi kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa jitihada za kulinda mazingira na kukuza utalii wa ikolojia.
Ziara hiyo imefanyika jana, Julai 12, 2025, ikihusisha Maafisa kutoka Makao Makuu ya TFS wakiongozwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi ambaye pia ni Mhasibu Mkuu wa TFS, pamoja na Maafisa wengine kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Ujumbe huo ulipokelewa na Mhifadhi Mkuu wa Shamba hilo, Robert Faida, ambaye aliwaongoza wageni kutembelea maeneo mbalimbali, ikiwemo kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la utawala na kushuhudia shughuli za uhifadhi wa mazingira na utalii wa ikolojia zinazotekelezwa ndani ya shamba.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Bw. Mwaisemba alieleza kuridhishwa na kasi ya ukusanyaji mapato na usimamizi wa rasilimali za misitu kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi hizo ili kufikia malengo ya makusanyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
βJuhudi mnazozifanya hapa zinaonyesha dhamira ya kweli ya kulinda misitu na kukuza utalii wa kiikolojia, sambamba na kuongeza mapato kwa serikali. Ni vyema mkahakikisha mipango hii inaendelea kwa ufanisi,β alisema Bw. Mwaisemba.
Kwa upande wake, Kamanda wa Kanda ya Kaskazini na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, James Nshare, alisema TFS imeanza kutekeleza miradi mipya kama vile biashara ya utomvu na hewa ya ukaa (carbon credits) ili kuongeza vyanzo vya mapato na kuimarisha mchango wa sekta ya misitu katika uchumi wa taifa.
βMiradi hii inalenga kuongeza mapato ya ndani na kutoa ajira kwa wananchi wanaozunguka mashamba haya. Vilevile, maboresho ya miundombinu tuliyoanza kufanya yataongeza ufanisi wa kazi na idadi ya watalii wanaotembelea shamba letu,β alisema Nshare.
Shamba la Miti West Kilimanjaro ni miongoni mwa mashamba ya miti makubwa yanayosimamiwa na TFS, likiwa na jukumu la msingi la uzalishaji wa mbao, uhifadhi wa mazingira na kukuza utalii wa kiikolojia katika Mkoa wa Kilimanjaro na maeneo jirani.
Β