Katika kuhakikisha Uchaguzi Mkuu 2025 unafanyika kwa usalama na amani Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kupitia watendaji wake wa kata limeendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali katika jamii, wakiwemo wasafirishaji wa abiria kwa kutumia Pikipiki maarufu kama bodaboda, kuhusu umuhimu wa kujiepusha kutumika vibaya kisiasa kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Akizungumza Julai 13, 2025 na wasafirishaji hao wa kijiwe cha Transfoma, katika ukumbi wa Karibu Tena uliyopo Kata ya Mwakakati Mji wa Tunduma Wilaya ya Momba, Polisi kata wa kata hiyo, Mkaguzi wa Polisi Robert Kasunga aliwahimiza wasafirishaji hao kujiepusha na vitendo vya fujo, ushawishi wa kisiasa wenye nia ovu, pamoja na usafirishaji wa watu wasiofuata sheria za kuingia nchini.
“Waendesha bodaboda mna nafasi kubwa sana katika jamii, lakini pia ni rahisi kutumika vibaya na watu wenye nia mbaya kisiasa. Nawaomba muwe makini, mchague usalama na amani kuliko tamaa ya fedha,” alisema Mkaguzi Kasunga.
Mkaguzi Kasunga, alisema kuwa kupitia vikundi vya Ulinzi Shirikishi na Viongozi wa Vijiwe vyote vya Bodaboda ndani ya kata hiyo kwa usimamizi wake ataendelea na mipango mikakati wa kuwachukulia hatua za kisheria dhidi ya yeyote atakayebainika kuhatarisha amani au kushawishi wengine kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani katika kata hiyo.
Aidha, bodaboda waliopata elimu hiyo walielezea kufurahishwa na hatua hiyo ya Jeshi la Polisi, wakisema kwamba imewafumbua macho na kuwapa uelewa zaidi wa wajibu wao katika kipindi cha uchaguzi.
“Tunaahidi kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha hakuna atakayetutumia vibaya na tuko tayari kuwa sehemu ya kulinda amani,” alisema Juma Mwampashi, mmoja wa bodaboda waliokuwepo.
Ikumbukwe kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linaendelea kutoa elimu ya masuala mbalimbali hasa yanayohusu usalama katika jamii ikiwa ni pamoja na elimu ya kushiriki uchaguzi kwa njia ya amani na kuepuka kushiriki vurugu au propaganda hatarishi.