Na mwandishi wetu, Simanjiro
Mwenge wa uhuru mwaka 2025 utakagua, kuzindua na kutembelea miradi 51 ya maendeleo yenye thamani ya Sh71.3 bilioni, katika mkoa wa Manyara.
Mkuu wa mkoa wa Manyara, Queen Sendiga ameyasema hayo mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro, wakati akikabidhiwa mwenge wa uhuru na mkuu wa mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi.
Sendiga amesema ukiwa katika mkoa wa Manyara mwenge wa uhuru utakimbizwa umbali wa kilomita 1,197.10 kwenye halmashauri saba za Simanjiro, Kiteto, Babati vijijini, Babati mjini, Mbulu mjini, Mbulu vijijini na Hanang’.
Amesema mwenge wa uhuru unaotarajia kuweka mawe ya msingi katika miradi 11 ya thamani ya Sh9.7 bilioni, kuzindua miradi 16 ya thamani ya Sh5.5 bilioni na kufungua mrad mmoja wa thamani ya Sh98.4 milioni.
Amesema mwenge wa uhuru utakagua na kuona miradi 23 ya thamani ya Sh55.9 bilioni na nguvu za wananchi Sh330 milioni.
Ameeleza kwamba katika fedha hizo Sh71.3 bilioni, serikali kuu imetoa Sh62.2 bilioni na mamlaka za serikali za mitaa kupitia mapato ya ndani imetoa Sh1.9 bilioni na wadau wengine Sh6.9 bilioni.
“Nawashukuru na kuwapongeza watu wa mkoa wa Manyara, kwa kuibua, kuanzisha, kuchangia na kuitekeleza miradi hiyo ya maendeleo,” amesema Sendiga.
Mkimbiza mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2025, Ismail Ussi amesema kauli mbiu ya mwaka huu ni jtokeze kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa amani.
“Mwaka huu wa 2025 tujitokeze kwa wingi kupiga kura za mgombea wa Rais, wabunge na madiwani ili tuweze kupata maendeleo zaidi kupitia hao,” amesema Ussi.