Wananchi mbalimbali waliotembelea banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea Viwanja vya Sabasaba Jijini Dar es Salaam, wametoa pongezi kwa huduma zinazotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakieleza kuwa zimekuwa zikiwasaidia kuelewa masuala ya kisheria na kuwapatia msaada wa changamoto mbalimbali.
Kwa upande wake Bw. Andrew Msanya akizungumzia huduma zinazotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amesema kuwa uwepo wa huduma za ushauri wa kisheria, elimu ya sheria na utatuzi wa changamoto mbalimbali umekuwa msaada mkubwa kwao, hasa kwa wale ambao hawakuwa na uwezo wa kupata huduma hizo kwa urahisi.
“Nimefika hapa kwenye banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, nilikuwa na changamoto ya masuala ya ajira nimepata maelezo mazuri na msaada wa kitaalamu kabisa, nimeelekezwa hatua za kuchukua”. Amesema Bw. Msanya.
Naye Bi. Suzan Abias ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutoa huduma za kisheria kwenye maonesho hayo kwani huduma hizo zitawasaidia wananchi wengi kufahamu haki zao.
“Nawashukuru Mawakili hawa kwa kutoa maelezo mazuri juu ya mambo ya kisheria, nawashauri wananchi wenzangu wenye changamoto za kisheria mje kwenye banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali msaidiwe”. Amesema Bi Suzan
Wakili wa Serikali Mwandamizi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Eneza Msuya ametoa wito kwa Wananchi kuendelea kutembelea banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika maonesho hayo ili wapate ushauri wa kisheria, elimu pamoja na utatuzi wa changamoto za kisheria zinazowakabili.
“Tunawakaribisha wananchi wote kwenye banda letu watumie fursa hii kupata huduma za ushauri wa kisheria, elimu ya sheria pia tunatatua na kushughulikia changamoto mbalimbali za kisheria, huduma hizi tunazitoa bila malipo.” Amesema Bw. Msuya
Banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali liko katika Hema la Jakaya Kikwete banda namba 24, Maonesho ya Sabasaba yaliyoanza tarehe 28 Juni, 2025 yanaendelea hadi Julai 13, 2025