Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WAKAZI 3,577 wa kijiji cha Nadonjuki kata ya Komolo wilayani Simanjiro mkoani Manyara, waliokuwa na changamoto ya kufuata maji umbali mrefu wa kilomita 15 wameondokana na adha hiyo baada ya mwenge wa uhuru kuzindua mradi wa maji.
Mradi huo wa maji wenye thamani ya Sh614.9 milioni unawaondolea kero wakazi wa kijiji cha Nadonjuki ya kufuata maji umbali wa kilomita 15 hadi katika vijiji vya Komolo na Terrat.
Meneja wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) wilaya ya Simanjiro, mhandisi Joanes Martin amesema mradi huo wa maji Nadonjuki umegharimu Sh614.9 milioni.
Mhandisi Martin amesema Serikali kuu imetoa Sh560.5 milioni na Sh54.3 ni mchango wa wadau kwa ajili ya kufunga mitambo ya nishati ya jua.
Ameeleza kwamba mradi huo utapunguza umbali wa kuchota maji kwani watu wa eneo hilo hivi sasa watapata huduma ya maji umbali wa mita 400 hadi 1,000.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa kwa mwaka 2025 Ismail Ussi amewapongeza RUWASA kwa namna walivyofanikisha mradi huo itakaonufaisha jamii.
“Hongera sana meneja wa RUWASA wa mkoa wa Manyara mhandisi James Kionaumela na meneja wa wilaya Martin,” amesema Ussi.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Fakii Raphael Lulandala amesema wanaishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za mradi huu.
“Suala la kumtua mama ndoo kichwani limefanyika kwa vitendo kwa kuondoa kero ya kufuata maji umbali mrefu tofauti na sasa,” amesema Lulandala.
Mmoja kati ya wakazi wa kijiji cha Nadonjuki, Enjo Daniel amesema awali walikuwa wanakunywa maji yasiyo masafi wala salama ya korongoni eneo la Njoromaimai au Mukamba.
“Sasa hivi badala ya kuhangaika na maji tunafanya shughuli nyingine za kujiongezea kipato badala ya kufuata maji mbali,” amesema.
Mkazi mwingine Naitapwak Laizer amefurahia kupata huduma ya maji karibu tofauti na awali walikuwa wanafuata maji umbali mrefu.
“Hivi sasa tunapata maji kwa ukaribu na kuondokana na kero ya muda mrefu ya kutembelea kilomita 30 kwenda 15 na kurudi 15 kufuata maji,” amesema Laizer.