Na Prisca Libaga RAS Arusha.
Jumla ya walimu 120,000 wamefikiwa na elimu ya kifedha na uwekezaji nchini, chini ya mpango wa ‘Mwalimu Spesho’ unatekelezwa na benki ya NMB.
Walimu hao kutoka shule za msingi na sekondari wamepewa elimu hiyo ndani ya miaka 10 ya mpango huo wenye lengo la kuwapa elimu ya kifedha, fursa za uwekezaji, mikopo na maandalizi ya kustaafu.
Hayo yamesemwa na meneja mwandamizi wa idara ya wateja binafsi kutoka NMB makao makuu, Ally Ngingite katika kongamano la ‘mwalimu Spesho’ lililokutanisha zaidi ya walimu 220 wa shule mbalimbali Wilayani Karatu Mkoa wa Arusha.
Amesema kuwa kwa miaka 10 tangu kuanzishwa kwa mpango huo zaidi ya walimu 120,000 wamefikiwa na elimu hiyo yenye lengo la kuwajengea nidhamu ya matumizi ya kifedha, kuwaonyesha fursa za uwekezaji kwa fedha zao au mikopo inayotolewa na NMB.
“Lakini pia tunatoa elimu ya suluhu za changamoto zao mbalimbali za kifedha kwa ajili ya ustawi wao wa kiuchumi wa sasa na baadae wakistaafu”
Amesema kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kuona jinsi walimu wanateseka na mikopo kutoka taasisi zisizo rasmi na kuathirika kisaikololojia katika marejesho kutokana na masharti magumu yasiyotekelezeka ikiwemo riba kubwa.
Akifungua kongamano hilo, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Karatu Juma Hokororo amesema kuwa walimu wamekuwa waathirika wakubwa wa mikopo umiza na kuishukuru benki ya NMB kwa kuwafikia walimu wa Karatu na elimu hiyo.
“Elimu ya kifedha nadhani ndio ilikuwa tatizo, ndio maana matapeli walikuwa wanawatesa, sasa tumieni fursa hii ya Elimu na mikopo kuhakikisha mnachukua hatua mpya ya maisha na ustawi wa uchumi wenu” amesema.
Amewataka walimu hao kuepuka mikopo yenye masharti ya kuwadhalilisha na kushusha heshima ya taaluma yao ikiwemo inayotaka dhamana ya kadi ya benki wanayotumia kulipwa nazo mishahara.
Amewataka kuchukua mikopo hiyo katika taasisi zilizo rasmi na zinazotambulika lakini pia wazingatie masharti yake.
“Mikopo ya hovyo hovyo wala haiwezi kuwasaidia kiuchumi zaidi inawadidimiza kwa kuwafilisi mnaposhindwa kulipa, hivyo kuanzia sasa hivi anzeni kuzingatia taasisi zenye heshima na hadhi”
Ametumia nafasi hiyo kuipongeza benki ya NMB kwa huduma mbalimbali wanazotoa kusaidia serikali katika sekta ya afya, elimu na mazingira.
Nae Meneja wa NMB wilaya ya Karatu, Edgar Ninga, amesema kuwa elimu hiyo pia inawasaidia walimu kujua masuluhisho yao ya kifedha za kidigitali zinazotolewa na taasisi hiyo ili waweze kujihudumia mkononi bila ya kufuata Ofisi.
Mmoja wa walimu kwenye kongamano hilo, Matilda Mathiasi kutoka shule ya Karatu Sekondari amesema kuwa elimu hiyo ni muhimu kwao na itawasaidia kutatua changamoto mbalimbali za kifedha wanazopitia walimu nchini.