Na WAF Karachi, Pakistan.
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Aga Khan wameendelea kuboresha ushirikiano katika maeneo ya mafunzo kwa wataalam wa afya, utoaji wa huduma za tiba, matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za tiba ili kuleta ufanisi zaidi wa ubora wa huduma za afya.
Hayo yanajiri baada ya Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe akiwa ameongozana na wa Wataalamu wa Sekta ya Afya kutoka Tanzania kufanya ziara nchini Pakistan ambapo Julai 14, 2025 wametembelea Hospitali na Chuo Kikuu cha Aga Khan kilichopo katika Jiji la Karachi.
“Ziara hii ni hatua ya kuanza kwa utekelezaji wa vipaumbele vya bajeti ya mwaka 2025/2026 ambayo iliwasilishwa na Mhe. Jenista Mhagama Waziri wa Afya Bungeni ambavyo ni pamoja na kuimarisha upatikanaji na Ubora wa Huduma za Afya zinazotolewa katika ngazi zote kuanzia zahanati hadi hospitali ya Taifa,” amefafanua Dkt Magembe.
Amesema ziara hiyo itaimarisha uhusiano na ushirikiano katika maeneo ya mafunzo kwa wataalam wa Afya, utoaji wa ithibati za ubora wa huduma za afya, utumiaji wa teknolojia katika utoaji wa huduma za afya hasa ngazi ya msingi na tiba utalii.
Dkt. Magembe amepokelewa na mwenyeji wake Dkt. Sulaiman Shahabuddin, ambaye ni Rais wa Chuo na Hospitali ya Aga Khan, yenye makao makuu yake Karachi Pakistan na kutembelea maeneo mbalimbali ya Hospitali, Chuo pamoja na kukutana na wataalam mbalimbali wa tiba na mafunzo, kubadilisha uzoefu na kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano kwa manufaa ya pande zote hususan katika kuimarisha ubora na mazingira ya kujifunzia ya watumishi wa afya kwa lengo la kuwawezesha kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.
Katika ziara hiyo Mganga Mkuu wa Serikali ameongozana na Mkurugenzi wa Mafunzo Dkt Saitore Laizer na Bi. Esther Msechu ambaye ni Afisa TEHAMA Mwandamizi na Simon Bwana Ernest ,Katibu wa Afya Mwandamizi.