KATIBU Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt.Fred Msemwa,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Julai 15,2025 jijini Dodoma kuelekea katika uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050,unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Julai 17,2025 jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIBU Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa,amesema mchakato wa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050,umekamilika na unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Julai 17,2025 jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dira hiyo ni muhimu kwani itakwenda kutoa mwelekeo wa maendeleo ya Tanzania kwa kipindi cha miaka 25 ijayo.
Dkt.Msemwa,ameyasema hayo leo Julai 15,2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea katika uzinduzi huo unaotarajiwa kuzinduliwa Julai 17,2025 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.
Amesema kuwa maandalizi ya Dira hiyo yamechukua karibu miaka miwili, yakihusisha ushirikishwaji mpana wa wananchi kutoka makundi mbalimbali.
“Tulipokea maoni kutoka kwa Watanzania takribani milioni 1.174 kupitia njia mbalimbali, na zaidi ya watu 20,000 walihudhuria makongamano ya kitaifa yaliyolenga kuibua maono ya pamoja kuhusu mustakabali wa Taifa letu,” amesema Dkt. Msemwa.
Hata hivyo amefafanua kuwa Tume ilifanya utafiti wa kina kwa nchi zilizofanikiwa kufikia uchumi wa kati ili kujifunza mbinu bora zinazoweza kutumika katika kufanikisha malengo ya Tanzania, hususan kujenga uchumi wa kati kwa njia endelevu.
Rasimu ya Dira hiyo ilirudishwa kwa wananchi kwa ajili ya uhakiki wa mwisho, kuhakikisha maoni yao yamezingatiwa. Baadaye, nyaraka hiyo ilijadiliwa na makundi ya kijamii, sekta binafsi, na wataalamu, ili kuhakikisha inawakilisha matakwa ya Taifa kwa mapana.
Aidha Dkt. Msemwa ameeleza kuwa utekelezaji rasmi wa Dira ya 2050 utaanza Julai 2026, mara baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2025.
Dkt. Msemwa,amesema kuwa Tume ya Taifa ya Mipango inaendelea kusimamia kwa karibu maandalizi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya muda mrefu ili kuhakikisha Tanzania inapata maendeleo shirikishi, jumuishi na endelevu kwa wananchi wote.