Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa William Mwegoha (kulia) akipata maelezo kutoka kwa Afisa Uhusiano wa Chuo hicho, Bi. Fatna Mfalingundi, wakati wa ziara yake iliyofanyika leo, Julai 15, 2025, katika kambi ya udahili ya mwaka wa masomo 2025/2026 iliyopo Mlimani City, Dar es Salaam. (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Afisa Uhusiano wa Chuo Kikuu Mzumbe kutoka Kampasi Kuu, Mkoa wa Morogoro, Bi. Fatna Mfalingundi akitoa elimu kuhusu huduma ya udahili katika kambi ya udahili ya mwaka wa masomo 2025/2026 iliyopo Mlimani City, Dar es Salaam.
Afisa Udahili wa Chuo Kikuu Mzumbe kutoka Kampasi Kuu, Mkoa wa Morogoro, Bi. Blandina Elisa (kushoto) akitoa huduma ya udahili katika kambi ya udahili ya mwaka wa masomo 2025/2026 iliyopo Mlimani City, Dar es Salaam.
Afisa TEHAMA Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam Alfred Mimata (kulia) akitoa huduma ya udhaili katika kambi ya udahili ya mwaka wa masomo 2025/2026 iliyopo Mlimani City, Dar es Salaam.
Afisa Udhaili Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam Aziza Suru akitoa elimu kuhusu huduma ya udhaili katika kambi ya udahili ya mwaka wa masomo 2025/2026 iliyopo Mlimani City, Dar es Salaam.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa William Mwegoha akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Chuo hicho katika kambi ya udhaili ya mwaka wa masomo 2025/2026 iliyopo Mlimani City, Dar es Salaam.
…….
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa William Mwegoha, amewaalika wanafunzi wote wanaotaka kujiunga na elimu ya juu waombe kujiunga na chuo kupitia msimu mpya wa udahili kwa mwaka wa masomo 2025/2026, ili waweze kuwa chachu ya maendeleo katika jamii na kuchangia kukuza uchumi wa Taifa.
Akizungumza leo, Julai 15, 2025, jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara yake katika kambi za udahili ambapo DSM kambi hiyo imewekwa maeneo ya Mlimani City, Profesa Mwegoha amesema kuwa Chuo kimeandaa timu maalumu ambazo zimepangwa katika mikoa mbalimbali nchini, kwa lengo la kusaidia wanafunzi kwenye mchakato wa udahili ili waweze kupata elimu bora itakayowawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Profesa Mwegoha ameongeza kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kinatoa programu mbalimbali za masomo kuanzia ngazi ya Astashahada hadi Shahada ya Uzamivu (PhD), kupitia kampasi zake zilizopo sehemu mbalimbali nchini.
“Nawakaribisha Watanzania wote kutembelea kambi zetu katika mikoa mbalimbali ili kupata taarifa kamili kuhusu udahili, kambi zetu zipo Dar es Salaam – Mlimani City, Mwanza – Rock City Mall, Dodoma – Nyerere Square, Arusha – Uwanja wa Makumbusho, pamoja na Mbeya – eneo la Kabwe,” amesema Profesa Mwegoha.
Ameeleza kuwa kwa sasa Chuo kinatumia mbinu rafiki na za kisasa katika ufundishaji ambazo zinawawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo na kuwa tayari kwa ajira hata kabla ya kuhitimu masomo yao.
Chuo Kikuu Mzumbe kinajivunia ubobezi wake katika taaluma mbalimbali zikiwemo Utawala, Biashara, Uchumi, Ujasiriamali, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), na Sheria, ambapo wahitimu wake wengi wamekuwa wakifanya kazi katika sekta za umma na binafsi ndani na nje ya nchi.
Profesa Mwegoha amewakaribisha Watanzania wote, hususan vijana waliomaliza elimu ya sekondari, kuomba kujiunga na Chuo hicho, kwani Chuo kipo tayari kuwapa elimu itakayowawezesha kujitegemea na kuchangia maendeleo ya Taifa, ambapo huduma katika mabanda hayo zitaendelea kutolewa hadi Julai 23, 2025.
“Chuo Kikuu Mzumbe, tujifunze kwa Maendeleo ya Watu”