Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Julai 15, 2025
Shule ya Msingi Mkoani yenye mchepuo wa Kiingereza, Kata ya Tumbi katika Manispaa ya Kibaha, mkoani Pwani, inakabiliwa na changamoto kubwa ya kifedha kutokana na wazazi kushindwa kulipa ada kwa wakati.
Shule hiyo ya serikali ilianzishwa mwaka 2018 kwa lengo la kutoa elimu bora kwa mchepuo wa Kiingereza kwa gharama nafuu, ikilinganishwa na shule nyingine binafsi, ili kuwapa watoto wa Kitanzania fursa sawa ya kielimu.
Hata hivyo, hali ya sasa inaonyesha kuwa wazazi wengi wameshindwa kulipa ada ya Shilingi 400,000 kwa mwaka, ambayo hugawanywa kuwa sh. 200,000 kwa kila muhula wa miezi sita, jambo linalohatarisha uendeshaji wa shule hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake,Julai 14,2025 Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Adelhelma Shawa, alisema shule hiyo inadai jumla ya Shilingi 168,956,000 kutoka kwa wazazi wa wanafunzi.
“Kati ya kiasi hicho, sh. 51,563,000 ni madeni ya miaka ya nyuma ambayo baadhi ya wazazi wamekuwa wakiyapunguza taratibu, lakini wengine bado wanaruhusu watoto wao kuendelea kuhudhuria masomo bila kulipa hata sehemu ya deni,” alisema Shawa.
“Nimekuwa nikiwaita wazazi kwa ajili ya vikao, tunakubaliana kwa maandishi kuwa atalipa tarehe fulani, lakini mara nyingi mzazi akitoka hapa shuleni hatumuoni tena,” alieleza Shawa.
Nae Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, alisema hakuna mwanafunzi ambaye amefukuzwa shule kwa sababu ya kutolipa ada, jambo ambalo baadhi ya wazazi wamechukulia kama sababu ya kutokulipa .
“Ukienda shule za binafsi, wanafunzi hawaruhusiwi kuingia darasani kama hawajalipa ada, lakini hapa Mkoani kwa kuwa ni shule ya serikali, wapo wazazi ambao hawajishughulishi kulipa ada kwa kuwa watoto wao hawafukuzwi,” alisema Dkt. Shemwelekwa.
Dkt. Shemwelekwa alieleza, shule hiyo inatakiwa kujiendesha kwa mfumo wa shule binafsi, na kwa sasa kuna mpango wa kuwaondoa walimu wote wa Serikali na kuajiri walimu wa moja kwa moja kupitia shule hiyo.
Aliongeza wazazi wanapaswa kutambua majukumu yao na kuthamini malengo ya shule hiyo, kwani ada ya sh. 400,000 kwa mwaka ni ndogo ikilinganishwa na shule binafsi zenye mchepuo wa Kiingereza ambazo huanzia sh. milioni mbili kwa mwaka.
Mmoja wa wazazi, Omari Salehe, ambaye mtoto wake anasoma katika shule hiyo, alisema uwepo wa shule hiyo ni msaada mkubwa kwao kwa kuwa mtoto anapata elimu bora kwa gharama ndogo ikilinganishwa na shule nyingine binafsi.