Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENGE wa uhuru umeipitisha na kuikubali miradi sita ya maendeleo iliyoitembelea kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara ya thamani ya shilingi bilioni sita.
Kutokana na hali hiyo Wilaya ya Simanjiro, imepata clean sheat na blu tick kupitia miradi yote ya maendeleo iliyokaguliwa na mwenge hakuna hata mmoja uliokataliwa na mwenge.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, mwalimu Fakii Raphael Lulandala ametaja miradi hiyo ni kuweka jiwe la msingi jengo la mionzi kituo cha afya Mirerani, kukagua kikundi cha ufyatuaji wa matofali Komolo na kuzindua mradi wa maji Nadonjukin.
“Miradi mingine ni kuzindua klabu ya afya na lishe, klabu ya kupinga na kupambana na rushwa katika shule ya sekondari Terrat, kutembelea, kukagua, kuona ujenzi wa shule ya sekondari Tukuta,” amesema Lulandala.
Pia, mwenye wa uhuru umepokea taarifa ya kikundi cha vijana cha Kiserian Namalulu na kukikagua, kuweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara ya bomani kwa kiwango cha lami mji mdogo wa Orkesumet na kukagua usafi wa mazingira soko la Orkesumet.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2025, Ismail Ussi amewapongeza viongozi na wananchi wa Simanjiro kwa namna walivyoutendea haki mwenge wa uhuru.
“Simanjiro hongereni sana DC wenu Lulandala mtu bingwa kabisa, DAS Warda Abeid Maulid dada lao, DED Gracian Max Makota kaka lao Rais Samia Suluhu Hassan mama lao,” amesema.
Amewapongeza Simanjiro kwa miradi mingi ya maendeleo iliyotembelewa na mwenge katika sekta ya afya, elimu, maji, miundombinu ya barabara na vikundi vya vijana vijana na wanawake vilivyopatiwa mikopo.
Mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa kupitia Wilaya ya Simanjiro, Lenana Lenganasa Soipey ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha miradi mingi ya maendeleo katika eneo hilo.
Lenganasa ameeleza kwamba ameshiriki mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2025 katika wilaya ya Simanjiro na kushuhudia miradi mbalimbali ya maendeleo ikipitiwa na mwenge.