MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian ,akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 15,2025 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi April 2025.
MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian ,akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 15,2025 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi April 2025.
SEHEMU ya Waandishi wa habari wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian (hayupo pichani) wakati akizungumzia Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi April 2025.
Na Alex Sonna-DODOMA
BANDARI ya Tanga imeboreshwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 429.1, hatua iliyoongeza idadi ya meli kutoka 198 hadi 307 kwa mwaka na kuboresha ufanisi wa kushusha mizigo kutoka siku 5 hadi siku 2 pekee.
Maboresho haya yameleta ajira, mapato kwa halmashauri na kusisimua biashara zinazohusiana na usafirishaji.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, ameeleza hayo leo JulAI 15,2025 Jijini Dodoma na kueleza kuwa serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa kwenye miradi ya msingi yenye lengo la kuifanya Tanga kuwa kitovu cha biashara, utalii, michezo, na huduma za kijamii.
Amesema Tanga pia ni mwenyeji wa mradi mkubwa wa bomba la mafuta (EACOP) kutoka Uganda, unaopita kwa urefu wa kilomita 205.91 ndani ya mkoa huo. Mradi huu umewezesha fidia ya zaidi ya shilingi bilioni 9.3 kwa wananchi waliopisha ujenzi, na kuwajengea nyumba mpya 43.
Amesema Zaidi ya ajira 810 zimetolewa katika eneo la Chongoleani pekee huku biashara ndogo kama mama lishe, huduma za usafirishaji na malazi zikikua kwa kasi.
Kwa upande wa vijana na vipaji, Mkoa umejivunia mradi wa ujenzi wa Kituo cha Michezo cha TFF – Mnyanjani, unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 4.5. Kituo hicho kitasaidia kukuza vipaji vya soka na michezo mingine, huku kikitengeneza ajira na mapato kupitia sekta ya burudani.
Hali kadhalika, Tanga imewekeza kwenye ujenzi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan Business Centre, jengo la kibiashara la kisasa lenye lengo la kuwakusanya wafanyabiashara wakubwa na wadogo, kuongeza ushindani wa huduma na kuongeza mapato ya halmashauri. Soko jipya la machinga pia linaendelea kujengwa kwa ajili ya kusaidia vijana na wamachinga kufanya biashara katika mazingira bora na salama.
Kwa upande wa ustawi wa jamii,amesema Mkoa wa Tanga kupitia mpango wa TASAF umewezesha zaidi ya walengwa 38,952 kuanzisha biashara ndogondogo, 48,645 kujiunga na bima ya afya na zaidi ya 44,000 kuingia kwenye sekta ya kilimo na ufugaji wa kisasa. Hii ni hatua kubwa kuelekea uchumi jumuishi unaogusa watu wa kawaida.
Zaidi ya hayo ameeleza kuwa Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya ukarabati wa kivuko cha MV Tanga, kinachotumika kusafirisha watu na bidhaa kati ya maeneo ya mwambao. Huduma hii inatazamwa kama kichocheo kipya cha utalii wa baharini na biashara ya ndani kwa ndani.
Katika kuhakikisha utawala bora na usimamizi wa rasilimali,amesema Mkoa umeongeza mahakama za mwanzo kutoka 65 hadi 67 na wilaya kutoka 6 hadi 8, huku ofisi za wakurugenzi na nyumba za viongozi zikiendelea kujengwa kwa usimamizi wa serikali kuu.