Mwandishi Wetu, Dar e Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amekutana na kufanya mazungumzo na wadau wa Biashara ya Kaboni kutoka nchini Korea ambao wameonesha nia ya kuja kuwekeza nchini katika biashara hiyo.
Kikao hicho kimefanyika Dar es Salaam, Julai 15, 2025 ambapo Waziri Masauni amesema ujio wa wadau hao ni matokeo ya ziara yake ya kikazi na Ujumbe wa Tanzania nchini Korea Kusini mwezi Machi, 2025 walipokwenda kujifunza mambo mbalimbali kuhusu biashara ya kaboni na kukutana na wadau kuelezea fursa zinazopatikana nchini.
Mhe. Masauni ameeleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi mwanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, Itifaki ya Kyoto na Makubaliano ya Paris.
“Nchi wanachama wana wajibu wa kutekeleza mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo upunguzaji wa gesijoto na kujenga uwezo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi na athari zake. Mikakati ya upunguzaji wa gesijoto inapaswa kufanyika ndani na nje ya nchi husika.”
Amesema Nchi ya Korea Kusini ni mojawapo ya nchi ambazo zinafanya vizuri katika biashara ya Kaboni. Kwa kuzingatia hali hiyo, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) iliandaa ziara ya mafunzo nchini Korea kwa lengo la kujionea na kujifunza kuhusu uzoefu wa usimamizi na uendeshaji wa biashara ya Kaboni, ziara ambayo sasa imeanza kuleta matunda.
“Moja ya lengo ya ile ziara ilikuwa kutangaza fursa zilizopo katika uwekezaji wa miradi ya Kaboni nchini, pamoja na kuchangamkia fursa mbalimbali za kifedha, masoko na utaalamu katika eneo la mabadiliko ya Tabianchi hususani kwenye biashara ya Kaboni.
“Katika ziara ile tulikutana na kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali ikiwemo Taasisi ya Huduma ya Misitu ya Korea ambao waliujulisha Ujumbe wa Tanzania kuwa ni kweli Tanzania inaweza kunufaika na dirisha la Subnational REDD+ projects kupitia Taasisi binafsi kama vile Good Neighbors.
“Good Neighbors walianza kufanya kazi siku nyingi nchini Tanzania kwenye miradi mingi ya kimaendeleo ambapo walitueleza wanaweza kusaidia katika kufanya upembuzi yakinifu wa miradi mbalimbali ya Kaboni ambao sasa wameambatana na wadau hao.” Amesema Mhe. Masauni.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Good Neighbors Tanzania Bi. Ilsun Jung amesema Tanzania imekuwa na fursa nyingi ndio maana wanahitaji kuwekeza katika biashara hiyo lakini kwa kufuta taratibu zinazotakiwa na serikali.
“Mradi upo katika hatua za awali za kubaini maeneo muhimu, changamoto kuu pamoja na kuweka mikakati ya kutekeleza shughuli zenye kuleta tija kwa serikali, jamii na wadau wengine watakaohusika. Lengo hadi mwaka ujao mradi uwe tayari.” amesema Bi. Jung.
Ameongeza kuwa mradi huu unaotarajiwa kutekelezwa mikoa ya Kigoma, Tabora, Singida, Iringa na Zanzibar huku Good Neighbors Tanzania ikiendelea kutafuta wadau muhimu, wenye nguvu ya rasilimali fedha na nia ya dhati katika kuendeleza mashirikiano yanayolenga kuleta maendeleo endelevu nchini Tanzania.
Hadi March 15, 2025 jumla ya maombi ya usajili wa miradi 72 ya Kaboni yalipokelewa katika Kituo cha Kitaifa cha Kuratibu Kaboni nchini (NCMC) kilichpo mkoani Morogoro) ambapo Sekta ya kilimo miradi saba (7), Mifugo (3), Misitu (33), Nishati (27) na Taka (2).