Na Silivia Amandius, Kagera
Shirika la Afya Duniani (WHO) limekabidhi vifaa vya afya kwa Mkoa wa Kagera vyenye thamani ya shilingi milioni 112, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uwezo wa mkoa huo katika kukabiliana na milipuko ya magonjwa hatari kama Marburg, ambao ulizuka miezi mitano iliyopita.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mwakilishi wa WHO nchini Tanzania, Dkt. Galbert Fedjo, alisema msaada huo ni sehemu ya juhudi za pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na washirika wa maendeleo katika kujenga mifumo madhubuti ya afya. Alisema Tanzania ilionesha uongozi na uthabiti mkubwa kwa kuudhibiti mlipuko wa Marburg ndani ya siku 60.
“Leo tunashuhudia hatua ya kuimarisha zaidi mfumo wa afya ili taifa liwe tayari kwa dharura zijazo. Ushirikiano huu ni mfano wa namna nchi zinavyoweza kujenga uimara kupitia mshikamano,” alisema Dkt. Fedjo.
Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Katibu Tawala wa Mkoa, Ndugu Steven Ndaki, alipokea vifaa hivyo na kutoa shukrani kwa WHO kwa mchango wao muhimu katika kuimarisha huduma za afya mkoani humo. Alisisitiza umuhimu wa vifaa hivyo kutunzwa na kutumika kwa uangalifu ili viweze kuwanufaisha wananchi kwa muda mrefu.
“Vifaa hivi vimegharimu shilingi milioni 112. Ni wajibu wetu kama mkoa kuhakikisha vinatunzwa vizuri na vinatumika kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla,” alisema Ndaki.
Msaada huo uliofadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia FCDO, unahusisha vifaa tiba, mafunzo kwa wahudumu wa afya, msaada wa afya ya akili na kisaikolojia kwa jamii zilizoathirika, pamoja na kuimarisha mawasiliano ya hatari wakati wa milipuko.
Dkt. Fedjo alihitimisha kwa kuipongeza Tanzania kwa kuonesha mfano wa kuigwa katika kudhibiti Marburg na kusisitiza kuwa WHO itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kila kituo cha afya, mhudumu wa afya na mwananchi anakuwa tayari kukabiliana na changamoto za kiafya.