Mkurugenzi Mtendaji Bw. Arumasi akifungua mkutano wa wateja wa Moshi.
Meneja Mpya wa Tawi la Moshi, Bi. Florentina Manyilizu alitambulishwa rasmi kwa wateja wakati wa kikao.
Wateja wakifuatilia kwa makini mafunzo ya elimu ya fedha yalitolewa wakati wa mkutano.
Picha ya pamoja ya wafanyakazi wa ACB na wateja wa Moshi, ikiashiria mshikamano na ushirikiano
AKIBA Commercial Bank Plc imeendelea kuimarisha dhamira yake ya kuwa benki inayosikiliza wateja kwa kufanya mkutano maalum na wateja wake jijini Moshi, tarehe 16 Julai 2025. Tukio hilo lilihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki, Bw. Silvest Arumasi, kama mgeni rasmi.
Mkutano huo uliwaleta pamoja wateja wa eneo la Moshi leo Julai 16, 2025kwa lengo la kusikiliza maoni yao, kushirikishana maendeleo ya Benki na kutoa elimu ya fedha. Pia ulikuwa ni jukwaa la kutoa shukrani kwa uaminifu wao tangu Benki ilipoanza kutoa huduma zake katika mkoa huo.
Bw. Arumasi aliwahimiza wateja kutumia majukwaa kama haya kama sauti yao ya moja kwa moja kwa Benki kwa kusema . “Kwetu ACB, kuwa karibu na mteja si kauli tu, ni utamaduni tunaouishi. Tunathamini maoni yenu na tumejizatiti kuyawekea kazi kwa vitendo,” alisisitiza.
Wateja walieleza mafanikio kadhaa ya ushirikiano wao na Benki na kutoa mapendekezo mbali mbali kwa lengo la kunufaisha pande zote mbili.
Aidha, wateja walionesha kufurahishwa kwa kiasi kikubwa na ushiriki wa moja kwa moja wa Mkurugenzi Mtendaji katika tukio hilo, hususan kwa kujibu hoja mbalimbali papo kwa papo na kutoa maamuzi ya moja kwa moja kwa baadhi ya changamoto zilizowasilishwa. Walimtaja kuwa kiongozi wa mfano mwenye upeo mpana wa kibiashara na uwezo wa kufikiri kimkakati, kipaji na uwezo unaosaidia kuharakisha maamuzi muhimu kwa maendeleo ya Benki na ustawi wa wateja.
Katika hitimisho la mkutano, Akiba Commercial Bank iliahidi kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na kuendeleza utamaduni wa kusikiliza wateja kama sehemu ya mkakati wake wa kuwa Benki inayosikiliza, inayojali na inayoleta matokeo chanya katika jamii.