NA MWANDISHI WETU
UONGOZI wa Chuo cha Ufundi cha Furahika kimetangaza kozi mpya ya kutengeneza sabuni ya maji na mche kwa wahitimu wa darasa saba, kidato cha nne na wale waliokatisha masomo ya Sekondari na Shule ya Msingi na watasoma bila ya malipo.
Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Dkt David Msuya, akizungumza leo, Julai 16, 2025 katika chuo hicho kilichopo Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam, amefafanua kuwa tayari dirisha la usahili limefunguliwa na fomu za kujiunga zinapatikana chuoni hapo au kwenye tovuti ambayo ni www.furahika college.co.tz.
“Watakacholipia wao ni fomu shilingi 50 pamoja na malipo ya mtihani unaosimamiwa na NACTVET kwa ajili ya kupata cheti ya kuhitimu kozi hiyo na nyinginezo ikiwemo, utengenezaji wa Keki, Biscuti, utengezaji Mishumaa, Hotel Management, Udereva, Umeme, Clearing Forward, Air Ticketing, Ususi, utunzaji mazingira na Malezi ya Watoto,” amesema.
Amesema lengo la kutoa elimu bure ni kuunga mkono juhudi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan na kumkomboa kijana ambaye alikwisha kata tamaa ya kuendelea na masomo kutokana na changamoto alizopitia ikiwemo kufiwa na wazazi.
Aidha amefafanua kwamba ni vema walezi ama wazazi wakatumia fursa hiyo kupeleka watoto katika chuo hicho kupata elimu na baada ya kuhitimu wanatafutiwa ajira itayowasaidia kujikwamua kiuchumi na kuondokana na kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya au biashara ya kuuza mwili.
Dkt Msuya amesema kozi hiyo na nyingine ikiwemo lugha ya kifaranza, kichina zitaanza katika muhula mpya wa masomo Agosti Mosi, 2025.