Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tathmini na Ufuatiliaji, Bi. Diana Kimario, akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 16,2025 jijini Dodoma kuhusu mafunzo ya kitaalamu ya siku tatu kuhusu usalama wa mabwawa ya majisafi na yale ya tope sumu (TSF) yanatarajiwa kufanyika jijini Mwanza kuanzia Novemba 19 hadi 21,mwaka huo.
Na.Meleka Kulwa-DODOMA
WIZARA ya Maji kwa kushirikiana na Chemba ya Migodi Tanzania (TCM) pamoja na Kampuni ya Uhandisi ya City, wanatarajia kuandaa mafunzo ya kitaalamu ya siku tatu kuhusu usalama wa mabwawa ya majisafi na yale ya tope sumu (TSF). Mafunzo hayo yanatarajiwa kufanyika jijini Mwanza kuanzia Novemba 19 hadi 21, 2025, yakiwa na kaulimbiu: “Tahadhari za Dharura za Kukabiliana na Majanga ya Mabwawa ya Maji na Tope Sumu.”
Hayo yamesemwa leo Julao 16,2025 jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tathmini na Ufuatiliaji, Bi. Diana Kimario,wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa mafunzo haya yamekuwa yakifanyika kila mwaka na mwaka huu yatafanyika kwa mara ya tatu mfululizo.
Bi. Kimario amesema kuwa lengo kuu ni kuongeza uelewa kwa wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi kuhusu usimamizi na uboreshaji wa usalama wa mabwawa, hasa yale ya migodini.
“Serikali imeendelea kuweka mkazo katika ushirikishwaji wa sekta binafsi, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutambua mchango wao katika maendeleo ya sekta ya maji na madini. “amesema Bi. Kimario
Aidha amesema kuwa Wizara itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau ili kuhakikisha mabwawa yote yanakidhi viwango vya usalama kwa mujibu wa Sheria ya Rasilimali za Maji.
Katika mafunzo hayo, wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kushiriki, jambo linalotoa fursa ya kubadilishana maarifa na uzoefu juu ya usimamizi salama wa mabwawa. Aidha, Bi. Kimario amewahimiza wadau wote wa mabwawa, ndani na nje ya Tanzania, kujitokeza kujiandikisha na kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji, Dkt. George Lugomela, ameonyesha wasiwasi juu ya hali ya baadhi ya migodi midogo ambayo bado inatiririsha majitaka kiholela, hali inayochangia uharibifu wa vyanzo vya maji. Ameeleza kuwa tofauti kubwa imeonekana kati ya migodi midogo na ile ya kati au mikubwa, ambapo migodi mikubwa inazingatia zaidi kanuni za usalama wa kimazingira.
Naye Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Migodi Tanzania (Tanzania Chamber of Mines-TCM) Benjamini Mchwampaka ameipongeza serikali kwa jinsi ambavyo imekuwa ikitoa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu. Amesema wataendeela kuwa pamoja ili kuhakikisha sekta ya maji na madini kwa ujumla zinakuwa na kuifikia jamii.
“Mafunzo haya yanatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha usalama wa mabwawa nchini na kupunguza hatari za kimazingira zinazotokana na mabwawa yasiyo salama, hususan yale ya migodini.”amesema