Na John Buukuku, Tabora
kurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TFDA) Dkt. Adam Fimbo, amesisitiza umuhimu wa kufanya majaribio ya dawa kabla hazijaanza kutumika kwa binadamu.
Akizungumza leo, Julai 16, 2025, katika kikao kazi cha wahariri wa vyombo vya habari na TMDA kilichofanyika mjini Tabora, Dkt. Fimbo amesema hakuna dawa inayopaswa kutumika kwa binadamu kabla ya kufanyiwa majaribio ya kina ya kisayansi.
Ameeleza kuwa hatua za awali huwa ni majaribio kwa wanyama wadogo kama panya, sungura hadi nyani, ili kubaini usalama na ufanisi wa dawa.
“Ni lazima ijaribiwe. Hatutaki kutumia dawa ambayo haijathibitika. Lengo ni kuhakikisha dawa inatibu na haina madhara kwa binadamu,” amesema Dkt. Fimbo.
Aidha, amefafanua kuwa si kila mtu anaruhusiwa kushiriki kwenye majaribio ya dawa, akitaja makundi kama wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, wafungwa na wanafunzi kuwa hawapaswi kuhusishwa.
“Ushiriki lazima uwe wa hiari na mtu mwenye akili timamu. Haiwezekani mtu kulazimishwa kujaribiwa bila ridhaa yake,” amesisitiza.
Dkt. Fimbo amesema kuwa mtafiti yeyote anayehitaji kufanya majaribio ya dawa hapa nchini, lazima apate kibali rasmi kutoka kwa mamlaka husika na atangaze hospitalini ili watu wajitokeze kwa hiari.
“Haiwezekani mtu aje Tabora, achukue watu na kuwapa dawa bila kufuata taratibu. Tunayo sheria na tunalinda usalama wa wananchi wetu,” amesema.
Pia, amezungumzia changamoto zinazokwamisha maendeleo ya kisayansi barani Afrika, ikiwemo hofu kubwa ya wananchi kuhusu majaribio ya dawa, tofauti na Ulaya ambako tafiti nyingi hufanyika kwa urahisi.
“Kuna watu wanaopinga hata matumizi ya wanyama kwenye majaribio, jambo linalozuia maendeleo ya tiba mpya,” amesema.
Kwa upande mwingine, Dkt. Fimbo amependekeza kuwepo kwa utaratibu rasmi ambapo vyombo vya habari vitapitia hatua ya kuomba kibali kabla ya kutangaza habari za utafiti au majaribio.
Pia ametoa wito kwa wataalamu wa TEHAMA kushirikishwa katika kuboresha mifumo ili kurahisisha utoaji wa vibali.