Mkazi wa mtaa wa Ndaoya kata ya Chongoleani eneo la Manyungu ambae ni mnufaika wa mradi wa EACOP Bwana Loita Naftali akisalimiana na mratibu wa kitaifa wa mradi kutoka TPDC Asiadi Mrutu alipomtembelea.
Bwana Loita Naftali akiwa kwenye pikipiki ambayo ni moja ya matunda ya fidia mradi wa EACOP.
………….
*Wananchi wampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mafanikio ya ujenzi wa Mradi, wafikia asilimia 64.2
* Timu ya wataalamu wa SULUHU wakutana na Uongozi wa Mkoa wa Tanga, kueleza mafanikio ya mradi
* Ajira kwa wazawa kipaumbele cha mradi kwa asilimia 80
*Mradi watumia Bilioni 10.4 kulipa fidia kwa wananchi wa Mkoa wa Tangai
Na Neema Mbuja, Tanga
Wananchi waishio kwenye vijiji vinavyopakana na mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki, EACOP wamesema Serikali ya awamu ya sita ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa ya kubadili maisha ya wananchi kiuchumi kupitia mradi wa bomba la EACOP kwa kufungua fursa za kiuchumi kwenye maeneo hayo.
Wananchi hao wameyasema hayo leo 16 Julai, 2025 kwa nyakati tofauti wakati walipokuwa wakielezea mafanikio ya utekelezaji wa mradi huo na kueleza namna ambavyo maisha ya mtu mmojammoja wamefanikiwa kufuatia uwepo wa mradi wa EACOP.
“ Sijawahi kuona mradi ambao umetoa manufaa makubwa ya kiuchumi na kubadili naisha ya wananchi wake kama huu wa EACOP na tunaishukuri sana Serikali ya Tanzania kukubali mradi huu kutekeleza” Alisema Bw. Loita Naftali mkazi wa kata ya Chongoleani
Amesema licha ya kujengewa nyumba, kupatiwa fedha za kujikimu kiasi cha shilingi 500,000 kwa mwezi, bado walipatiwa elimu ya ujasiriamali, Kilimo na ufugaji wa kisasa ili kuinua hali ya uchumi.
Naye, Kassim Mwavezo Mbega amesema tangu kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki EACOP mkoa wa Tanga umeimarika kiuchumi na mzunguko wa fedha kuwa mkubwa tofauti na ilivyokuwa hapo awali na kuongeza kuwa kwa sasa wimbi la ujenzi wa nyumba za wageni na za binafsi pamoja na taasisi za fedha umekuwa mkubwa kutokana na mkoa kupokea wageni wengi wa mradi wa EACOP.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa EACOP kutoka TPDC Asiadi Mrutu amesema wakati wa zoezi la awali la kuwafidia wananchi hao Mradi ulitekeleza mpango maalumu chini ya taratibu za Kimataifa wenye lengo la kuwapatia elimu ya ujasirimali na kuendeleza kilimo na ufugaji wa kisasa ili wajiendeshe kibiashara sambamba na elimu ya utunzaji wa fedha.
Amesema kupitia programu hii, imeboresha sana maisha yao na familia zao sambamba na upatikanaji wa ajira kwa wananchi wanaozunguka eneo la mradi.
Awali kabla ya kuzungumza na wananchi wanufaika wa mradi wa EACOP timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Nishati,na TPDC ,na TBC kwa ajili ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa EACOP na mafanikio yaliyopatikana kwa Serikali ya awamu ya sita, ilifika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga na kupokelewa na Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Tanga Bi Amina Kibunde Said na kuieleza timu hiyo kuwa mradi wa EACOP ni miongoni mwa miradi ya kimkakati na yq mfqno kitekelezwa hapa nchini kutokana na uwazi wa uendeshaji wa mradi huo.
Amesema uchumi wa Mkoa wa Tanga kwenye Wilaya zake 6 zinazopitiwa na mradi huo zimenufaika pia na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo maji, umeme na wananchi mmojammoja. na kuishukuru Serikali kwa kazi nzuri inayofanya utekelezaji wa miradi mbalimbali.
“ Niahidi kuwa mkoa utaendelea kutoa ushirikiano kwenye utekelezaji wa mradi huu kwani viijana wengi wamenufaika na mradi wa EACOP kwa kiasi kikubwa “ Alisema Bi. Amina
Amewashukuru Wizara ya Nishati kupitia TPDC kwa kuhakikisha wananchi wote wanafidiwa isipokuwa kwa wale 12 ambao wana changamoto binafsi ikiwemo za kifamilia na mirathi ambapo jumla ya shilingi Bilioni 10.4 zimetumika kulipa fidia sawa na asilimia 99.3.