NA FAUZIA MUSSA
NGALAWA ya Too Much imeibuka mshindi wa kwanza katika mashindano ya mbio za ngalawa yaliyofanyika katika Bahari ya Fumba, Shehia ya Fumba, huku mashindano hayo yakishuhudia ushindani mkubwa kutoka kwa washiriki tisa.
Mashindano hayo ni sehemu ya kurudisha michezo ya asili visiwani Zanzibar, yalivutia mamia ya wakazi wa Fumba na maeneo jirani, ambapo ngalawa ya Wape Kazi iliibuka mshindi wa pili, huku nafasi ya tatu ikinyakuliwa na ngalawa ya Ubaya Ubwela.
Nafasi ya nne ilichukuliwa na ngalawa ya Utoto Raha, ya tano Atoae Mola, ya sita Mungu Ibariki, ya saba Msihofu, ya nane Safiria Nyota Yako, na nafasi ya tisa ilikamilishwa na ngalawa ya Sio Wote.
Washindi hao waliweza kufika katika fukwe za Fumba, eneo la kituo cha umeme, ambapo mashindano yalihitimishwa kwa shamrashamra na nderemo kutoka kwa wakazi walioufurahia mchezo huo wa asili.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘B’ Amour Yussuf Mmanga alisifu mchango wa michezo katika kudumisha mshikamano na kueleza kuwa mashindano hayo ni daraja la kujenga umoja, urafiki na historia miongoni mwa wanajamii wa Fumba.
Alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani wakati wote, akieleza kuwa bila amani na utulivu, shughuli kama hizo haziwezi kufanyika kwa mafanikio.
Kwa mujibu wa Mratibu wa mashindano hayo, Mohammed Abdalla Mohammed, alifahamisha kuwa mashindano ya ngalawa yamerudishwa rasmi mwaka 2013 baada ya kusita kwa muda mrefu, na kwamba lengo kuu ni kuwaunganisha wananchi wa Njia Namba Saba na vijiji vya jirani kwa njia ya michezo ya asili.
Alieleza kuwa pamoja na changamoto kadhaa za kiutendaji, msaada kutoka kwa Legal Services Facility (LSF) na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria umesaidia kufanikisha mashindano hayo kwa mafanikio makubwa.
“Tunataka michezo ya asili kama hii idumu na kurithishwa kwa vizazi vijavyo. Ni urithi wa utamaduni wetu,” alisema Mohammed.
Kwa upande wake, Nahodha wa Too Much, Mahmoud Abdalla Juma, ambaye ndio aliongoza ngalawa hiyo hadi ushindi, alieleza kuwa siri ya mafanikio yao ni kujiegemeza kwa Mungu pamoja na uimara wa chombo chao kinachohimili mawimbi makali ya baharini.
“Mungu ndiye muongozaji wetu. Bila yeye tusingefanikiwa. Pia tunashukuru kwa mashindano haya ya kipekee ambayo yanatufanya tujisikie sehemu ya jamii yetu,” alisema nahodha huyo.
Mshindi wa kwanza alizawadiwa kitita cha shilingi 500,000 na cheti cha ushiriki, wa pili alipata shilingi 300,000 na cheti, huku mshindi wa tatu akiambulia shilingi 200,000 na cheti.
Mashindano hayo ni sehemu ya matukio ya wiki ya msaada wa kisehria na yametoa ujumbe mzito juu ya mshikamano, amani na utambulisho wa kitamaduni, na kwa hakika yameonesha kuwa michezo ya asili bado ina nafasi kubwa katika kujenga jamii yenye umoja na maelewano.