Ujumbe kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (OAG) ukiongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samwel M. Maneno, umetembelea makao makuu ya Benki ya NMB na kufanya kikao na uongozi wa benki hiyo ukiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu, Bi. Ruth Zaipuna.
Kikao hicho kilichofanyika katika makao makuu ya NMB jijini Dar es Salaam, kikilenga kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili, hususan katika kubadilishana uzoefu na mbinu bora za utoaji wa huduma kwa wateja.
Ujumbe wa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali uliambatana na viongozi mbalimbali wakiwemo Bw. Ipyana Mlilo – Mkurugenzi Msaidizi Uratibu, Bi. Leila Muhaji – Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Bw. Juma Mziray – Afisa TEHAMA Mwandamizi, na Bw. Nyamhanga Nyamhanga – Wakili wa Serikali.
Kupitia mazungumzo hayo, pande zote mbili zilitambua umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya umma na binafsi katika kukuza ufanisi wa utoaji huduma na kuleta maendeleo jumuishi.
Kikao hicho ni sehemu ya juhudi za pamoja za kuimarisha utawala bora na kuhimiza matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.