Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameitaja sekta ya madini kuwa ni miongoni mwa maeneo tisa ya kipaumbele katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025-2050 kutokana na mchango wake mkubwa katika uchumi wa nchi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi rasmi wa Dira hiyo mpya ya maendeleo uliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC) jijini Dodoma, Rais Samia ameeleza kuwa Sekta ya Madini ina nafasi muhimu katika kuchochea maendeleo ya sekta nyingine, kuongeza ajira kwa Watanzania, pamoja na kuinua pato la taifa kupitia uongezaji wa thamani wa bidhaa zinazozalishwa.
Aidha, Rasi Samia amesema, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025-2050 imetambua kwa kina umuhimu wa sekta ya madini katika kuendesha uchumi wa viwanda, kuimarisha biashara ya nje kwa kuuza bidhaa zilizoongezwa thamani, na kutoa ajira kwa vijana wengi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Aidha, Rais amebainisha kuwa lengo la Dira hiyo ni kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi imara, jumuishi na shindani kimataifa.
Kutokana na umuhimu huo, Serikali imejipanga kuondokana na mfumo wa kuuza malighafi ghafi nje ya nchi. Badala yake, itawekeza ,zaidi katika teknolojia na viwanda vitakavyoongeza thamani kwenye bidhaa za bidhaa ili kuongeza mapato na kukuza ajira.
Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025-2050 ni mwendelezo wa Dira ya Maendeleo ya 2025, na imeandaliwa kwa kuzingatia mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia duniani. Kupitia Dira hii mpya, serikali imelenga kufikia uchumi wa kati wa juu unaotegemea viwanda, maarifa, ubunifu na matumizi ya rasilimali kwa tija na uendelevu.
Sekta nyingine zilizopewa kipaumbele katika Dira hiyo ni pamoja na sekta ya Kilimo, Utalii, Viwanda, Sekta ya Ujenzi na mali isiyohamishika, Uchumi wa Bluu, sekta ya Michezo na Ubunifu, Huduma ya Fedha na Sekta ya Huduma.
Pamoja na mambo mengine, uzinduzi wa Dira ya Maendeleo 2050 umeweka msingi thabiti wa mkakati wa muda mrefu wa kuijenga Tanzania mpya, yenye maendeleo jumuishi na endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.