


Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Nyanda Shuli akizungumza na wadau wa sekta ya wavuvi wadogo wakati akifunga mkutano maalum wa wadau wa sekta ya uvuvi leo, Julai 17, 2025, katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam. (PICHA NA NOEL RUKANUGA)


Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Nyaraka THBUB, Bi. Jovina Muchunguzi akiwasilisha mada kwenye
mkutano maalum wa wadau wa sekta ya uvuvi leo, Julai 17, 2025, katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam.

Afisa Uvuvi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Erica Mbiling’i akiwasilisha mapendekezo ya wadau wa sekta ya wavuvi wadogo kwenye mkutano maalum wa wadau wa sekta ya uvuvi leo, Julai 17, 2025, katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam.






Picha za matukio mbalimbali.
………………
Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Nyanda Shuli, amewataka wavuvi wadogo, maafisa uvuvi, pamoja na wadau wengine wa sekta ya uvuvi kuweka mipango rafiki na endelevu kwa ajili ya kutekeleza kwa vitendo maazimio yote yaliyojadiliwa katika mkutano maalum wa wadau wa sekta ya uvuvi.
Mkutano huo umelenga kukuza uelewa wa pamoja kuhusu haki za binadamu katika muktadha wa upatikanaji na usimamizi shirikishi wa rasilimali za baharini kwa wavuvi wadogo.
Akizungumza wakati akifunga mkutano huo leo, Julai 17, 2025, katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam, Kamishna Shuli amesema kuwa tume ina majukumu mbalimbali ikiwemo kusikiliza, kuchunguza na kufuatilia masuala yanayohusu haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha utekelezaji wa haki hizo unafikiwa kwa ufanisi.
“Katika haki za binadamu, tunaamini hakuna haki ndogo kwani zote ni muhimu na zinapaswa kulindwa. Linapokuja suala la ulinzi, ufuatiliaji na utetezi wa haki, tunapaswa kuwa makini kwa sababu mambo haya yanagusa maisha ya watu na mustakabali wa haki zao,” amesema Kamishna Shuli.
Aidha, amewashukuru washiriki wa mkutano huo kutoka mikoa mbalimbali pamoja na viongozi kutoka mashirika ya umma na sekta binafsi, wakiwemo wawakilishi wa Taasisi ya Haki za Binadamu ya Denmark na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kwa ushiriki wao wenye tija.
Kwa upande wake, Afisa Uvuvi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Erica Mbiling’i, amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wavuvi wadogo katika miradi ya uhifadhi wa mazingira ya bahari, pamoja na kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu ili waweze kukabiliana na changamoto zinazowakumba.
Mkutano huo wa siku mbili, uliofanyika kuanzia Julai 16 hadi 17, 2025, umeandaliwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kushirikiana na Taasisi ya Denmark ya Haki za Binadamu ukiwa na lengo la kukuza uelewa wa pamoja kuhusu haki za binadamu zinazohusiana na upatikanaji na usimamizi wa pamoja wa rasilimali za bahari kwa wavuvi wadogo.
Washiriki wa mkutano walipata fursa ya kujadiliana kwa kina, ikiwa ni pamoja na kuandaa muhtasari wa kitaifa wa mijadala, kubaini mbinu bora za kukabiliana na changamoto zinazowakabili wavuvi wadogo, pamoja na kupendekeza suluhisho jumuishi.
Mkutano huo pia ulijadili haki za wavuvi wadogo katika upatikanaji wa rasilimali za bahari na usimamizi wake, huku ukiwakutanisha pamoja wawakilishi kutoka Serikali, asasi za kiraia, vyama vya wavuvi, wataalamu wa mazingira ya bahari, pamoja na mashirika ya kimataifa yanayojihusisha na maendeleo ya sekta ya uvuvi.