Mkurugenzi wa shirika hilo Livingstone Masija akizungumza wakati wa utoaji wa mafunzo hayo jijini Arusha
……
Happy Lazaro, Arusha .
Arusha .SHIRIKA la ustawi wa wanyama Tanzania (ASPA) lenye makao yake makuu mkoani Arusha limeendesha semina kwa wanahabari kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutambua umuhimu na thamani ya mnyama Punda katika jamii.
Mkurugenzi wa shirika hilo Livingstone Masija akizungumza wakati wa utoaji wa mafunzo hayo amesema kuwa shirika hilo limekuwa likitetea hali za wanyama.
Amesema kuwa, takwimu zinaonyesha kuwa Punda 150 hutoroshwa kila mwezi kutoka nchini na kupitishwa katika mpaka wa Namanga kwa kuwapakia kwenye malori au kwa kutumia njia ya kuwaswaga kama vile wanawachunga.
Aidha Masija amesema jitihada mbalimbali zinahitajika kwa serikali,jamii pamoja na taasisi mbalimbali kuhakikisha zinamlinda mnyama huyo ambaye ni nguvu kazi nchini huku akipongeza jitihada za serikali kutambua thamani ya mnyama huyo kwa kuvifungia viwanda vya kuchinja Punda.
Aidha imeiomba serikali pamoja na wadau wa wanyama hapa nchini kuongeza jitihada za kukabiliana na ukatili dhidi ya mnyama Punda anayetishia kutoweka hapa nchini kutokana na uwepo wa biashara haramu ya nyama hiyo na wimbi la utoroshaji kwenda nchi jirani.
“Takwimu zinaonesha kuwa takribani punda 150 hutoroshwa kila mwezi kutoka nchini kupitia mpaka wa Namanga kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo kuwapakia kwenye Malori au kutumia njia ya kuwaswaga kama wanachungwa”amesema Masija .
“Tumekutana hapa kujaribu kuangalia ustawi wa Punda kwa ujumla jinsi ambavyo wamekuwa wakiteswa, kuibiwa na kuchinjwa ili kuboresha faida za punda kwa ujumla .”amesema .
Ameongeza kuwa , licha ya jitihada za Serikali pamoja na Taasisi mbalimbali zinazotetea ustawi wa wanyama mkoani hapa bado jitihada zaidi zinahitajika ili kukomesha uchinjaji na utoroshaji wa Punda kunakotishia kutoweka kwa mnyama huyo nguvu kazi hapa nchini.
“Punda asionekane kama ni nguvu kazi ya kusaidia watu masikini tu bali hata wenye uwezo, tuangalie faida ya Punda na jinsi gani tufanye ili kuboresha maisha ya Punda kwa ujumla” amesema
Aidha Masija aliishukuru serikali kwa kuvifunga viwanda vya kuchinja Punda vilivyokuwa katika Mikoa ya Dodoma na Shinyanga baada ya kuvipatia vibali vya kuchinja punda 30 kwa siku lakini badala yake viwanda hivyo vilichinja hadi Punda 100 kwa siku jambo ambalo lilitishia kutoweka kwa raslimali hiyo.
“Serikali imezuia Biashara ya Punda hapa nchini lakini bado kuna wimbi la utoroshaji wa wanyama hao kupitia mpaka wa Namanga. Ninachoomba sisi sote tushirikiane kukomesha wimbi hilo” amesema.
Serikali imezuia Biashara ya Punda hapa nchini lakini bado kuna wimbi la utoroshaji wa wanyama hao kupitia mpaka wa Namanga,ninachoomba sisi sote tushirikiane kukomesha wimbi hilo” amesema.