Na Fauzia Mussa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesems itaendeleza juhudi thabiti za kuhakikisha wananchi wote wanapata haki kwa usawa na kwa wakati, ikiwa ni sehemu ya ajenda yake ya kujenga jamii yenye misingi ya haki, usawa na maendeleo jumuishi.
Akizungumza katika ufunguzi wa Jukwaa la Tano la Mwaka la Msaada wa Kisheria lililofanyika ukumbi wa ZSSF Michenzani Mall Katika wiki ya msaada wa kisheria, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shaaban Ramadhan Abdalla, alisema kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa taasisi zote zinazojihusisha na utoaji wa msaada wa kisheria.
“Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa taasisi na wadau wanaotoa msaada wa kisheria kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kwa usawa,” alisisitiza Abdalla.
Alieleza kuwa serikali imejidhatiti kufanya ufuatiliaji na tathmini ya huduma hizo ili kuhakikisha zinafikiwa kwa weledi, uwazi na ufanisi bila ubaguzi.
Aidha aliipongeza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, ambapo kwa upande wa Zanzibar zaidi ya wananchi 422,908 wamenufaika wakiwemo wanaume 213,723 na wanawake 290,185 huku migogoro 749 ikiripotiwa na 259 kati yake kutatuliwa papo hapo.
Abdalla alieleza kuwa huduma hizo zimepunguza migogoro ya kijamii ikiwemo migogoro ya ardhi, ndoa, mirathi, ajira na udhalilishaji wa kijinsia, hasa kwa wale wasiokuwa na uwezo wa kulipia huduma za kisheria na kusisitiza kuwa wasaidizi wa sheria wana nafasi muhimu katika kufanikisha haki jumuishi.
Kwa upande wake, Bakari Omar Hamad kutoka Legal Services Facility (LSF), alisisitiza kuwa mafanikio ya msaada wa kisheria hayawezi kufikiwa bila ushirikiano wa karibu kati ya serikali, jamii na wadau wa huduma hizo.
“Huduma hii haiwezi kufika kila kaya bila ushirikiano thabiti. LSF itaendelea kushirikiana na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa,” alisema.
Dk. Sikujua Omar Hamdan aliwasilisha mada kuhusu umuhimu wa ufuatiliaji na tathmini katika kuimarisha huduma za Msaada wa kisheria alieleza kuwa nyenzo hizo husaidia kubaini mafanikio, changamoto na kuweka mikakati madhubuti kwa maendeleo endelevu.
Slisisitiza umuhimu wa takwimu sahihi kwa ajili ya kufanya maamuzi ya kisera, kuweka mipango ya maendeleo, na kuongeza uwajibikaji wa watoa huduma. umuhimu wa takwimu sahihi kwa ajili ya kufanya maamuzi ya kisera, kuweka mipango ya maendeleo, na kuongeza uwajibikaji wa watoa huduma.
Wasaidizi wa Sheria walitaja changamoto kama ukosefu wa rasilimali fedha, vifaa, pamoja na mahudhurio hafifu ya wananchi kwenye mikutano ya uhamasishaji.
Shaaban Sarboko Makarani Mkurungezi wa wasaidizi wa sheria Wilaya ya Kaskazini ‘B’ alitoa wito kwa wadau kuunga mkono jitihada hizo ili huduma hiyo iweze kuwafikia wananchi wote, hasa wa maeneo ya vijijini.
Mtumwa Ameir Ali kutoka Shirika la Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu Zanzibar, alishauri kufanyika kwa mikutano ya mara kwa mara kati ya wasaidizi wa sheria na taasisi za serikali kwa ajili ya tathmini na kupanga mikakati ya pamoja.
Salma Saadat, Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wenye Ulemavu, alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu kama vile wakalimani wa lugha ya alama katika huduma hizo.
Jukwaa hilo lililoandaliwa na LSF Kwa kushirikiana na Idara ya Katiba na msaada wa kisheria lilihudhuriwa na watoa huduma wa msaada wa kisheria kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, likiwa na kaulimbiu: “Ufuatiliaji na tathmini husaidia kuimarisha ubora na ufanisi wa huduma za msaada wa kisheria.”
Mada zilizowasilishwa zilijikita katika nafasi ya ufuatiliaji na tathmini, matumizi ya takwimu sahihi na umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii katika utoaji wa huduma hizo.