FWITC-MAFINGA KUENDELEA KUTOA MAFUNZO YA KINA KWA WATAALAMU WA MISITU
Na Mwandishi Wetu, Mafinga
Chuo cha Mafunzo ya Misitu na Viwanda vya Misitu (FWITC), kilichopo Mafinga mkoani Iringa, kimeendelea kuwa kichocheo kikubwa cha kuandaa wataalamu mahiri katika sekta ya misitu na viwanda vinavyotegemea misitu nchini.
Hayo yamebainishwa wakati wa ziara ya baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii chuoni hapo, ambapo Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Abdalla Mvungi, amesisitiza kuwa mafunzo yanayotolewa katika chuo hicho yanapaswa kuendana na mabadiliko ya kisasa na teknolojia za kisasa ili kuongeza tija kwa wahitimu.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mvungi amesema: “Tunataka kuona wanafunzi wanaohitimu hapa wanakuwa chachu ya mabadiliko katika jamii, wakibadilisha taswira ya biashara ya miti kwa vitendo na kuleta matokeo chanya. Hii itasaidia kuchochea maendeleo endelevu ya sekta ya misitu na viwanda vinavyotokana nayo.”
Amesisitiza kuwa ni lazima chuo hicho kitoe mafunzo yatakayowatofautisha wanafunzi wake na watu wasio na elimu ya kitaalamu katika nyanja hiyo na kwamba bidhaa zinazozalishwa kupitia mafunzo ya FWITC, zikiwamo mbao na thamani nyingine, zinapaswa kuwa bora zaidi na zenye viwango vya kimataifa.
Naye, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Freman Masawe, amesema tangu kuanzishwa kwake, chuo hicho tayari kimezalisha jumla ya wanafunzi 97 waliopata mafunzo ya muda mrefu katika nyanja mbalimbali, ikiwemo uanzishaji na utunzaji wa vitalu vya miche ya miti, uanzishwaji wa mashamba ya miti, pamoja na mbinu za kudhibiti majanga ya moto wa msituni.
Masawe amefafanua kuwa kwa wanafunzi wa muda mfupi, chuo kinatoa mafunzo ya ukarabati wa misumeno ya mikanda, matumizi sahihi ya misumeno ya minyororo, mbinu za uvunaji miti kwa tija, uchakataji wa magogo, ukaushaji mbao, pamoja na uwekaji wa dawa kwenye mbao na nguzo za umeme.
Aidha, amesema chuo hicho pia hufundisha mbinu za uzalishaji wa mkaa na nishati mbadala ili kuhamasisha matumizi ya nishati endelevu inayosaidia kuhifadhi mazingira.