Na Mwandishi wetu, Mbeya
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Erica Yegella amewataka walimu wa shule za awali na msingi kuhakikisha wanawajibika ipasavyo kwa kuweka misingi mizuri na imara katika suala zima la ufundishaji kwa watoto kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi kuwa na uelewa wa kujua kusoma, kuandika pamoja na kuhesabu lengo ikiwa ni katika kuboresha sekta ya elimu kuanzia ngazi za chini.
Yegella ameyasema hayo wakati wa halfa ya ugawaji wa madawati 50 katika shule mbili za msingi ikiwemo jitegemee pamoja na shule ya msingi ya Mlimareli zilizopo katika kata ya Utengule Usongwe ambayo yametolewa kwa msaada wa benki ya CRDB ikiwa ni katika kuunga juhudi za serikali ya awamu ya sita katika kuboresha kiwango cha elimu.
Mkurugenzi huyo amesema kwamba watoto wote ambao wanasoma katika elimu ya awali pamoja na wale wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili pindi anapoingia kufanya mitihani yake anapaswa awe tayari anafahamu kusoma, kuandika, na kuhesabu hivyo walimu wanapaswa kulivalia njuga suala hilo ili kuongeza kiwango cha elimu kwa wanafunzi hao.
Aidha Mkurugenzi huyo amebainisha kwamba madawati hayo yataweza kuwa mkombozi mkubwa kwa wanafunzi hao kuweza kuondokana na adha ya kusoma wakiwa katika mlundikano na kwamba wataweza kusoma katika mazingira ambayo ni rafiki zaidi na yataleta mabadiliko chanya ya kimaendeleio katika nyanja hiyo ya elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.
“Kwa kweli kwa upande wangu mimi kama mkurugenzi nipende kushukuru sana benki ya CRDB kwa kuweza kukubali amaombi yetu ya kutusaidia madawati haya 50 ambayo tutaweza kuyagawanya katika shule mbili na nina imani yataweza kuwa msaada mkubwa kwa watoto wetu ambao ni wanafunzi wa shule mbili,”amesema Mkurugenzi huyo.