*Awataka Wakandarasi kuongeza kasi ili Miradi ikamilike kwa wakati.
*Asema lengo la TANESCO ni kuhakikisha inamudu mahitaji ya wateja wake
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange Julai 18, 2025 amefanya ziara ya kuagua maendeleo ya Miradi ya umeme ukiwemo wa Njia ya kusafirisha umeme kutoka Zuzu hadi Mbande, Mradi wa kusambaza umeme ardhini katika mji Serikali na Mradi wa Kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Mjini Mkoani Dodoma.
Bw. Twange ameelezea maendeleo ya Mradi wa njia ya kusambaza umeme wa Msongo wa Kilovolti 33 kutoka Mbande hadi Zuzu kwamba umefikia asilimia 48.35 huku Mradi wa usambazaji wa umeme ardhini kwenye mji wa Serikali Ihumwa ukifikia asilimia 64 ambapo hadi kukamilika kwake utagharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 50.09 ambapo amewataka Wakandarasi kuongeza kasi ili Miradi hiyo ikamilike kwa wakati na ianze kuwahudumia wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji huyo pia amekagua maendeleo ya Mradi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Mjini Dodoma ambacho kimefikia zaidi ya asilimia 80 na kinatarajia kukamilika rasmi mwanzoni mwa mwezi Septemba Mwaka huu.
‘’Kituo cha kupokea umeme cha mjini kimefikia zaidi ya asilimia 80, nataka kuwaeleza kuwa mwanzoni mwa mwezi wa tisa Kituo hiki kitakamilika. Kituo hiki kitatupa uwezo wa kuwasambazia umeme wateja wetu walioko Katikati ya mji kwa kuwa kituo kilichokuwepo awali kilizidiwa na tunachotaka ni kumudu mahitaji ya wateja wetu, alifafanua Bw. Twange.
Aidha, Bw. Twange amesema licha ya changamoto za kifedha zilizojitokeza kwa baadhi ya miradi amewapongeza wasimamizi wa Miradi kutoka TANESCO na Wakandarasi ambapo ameeleza kuwa kukamailika kwa miradi hiyo kutachangia upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma na maeneo Jirani ya Mkoa wa Morogoro.