NA EMMANUEL MBATILO, PWANI
MWENYEKITI wa Bodi ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Profesa Aurelia Kamuzora amesema kutokana na uhitaji mkubwa na uwezo wa kurudisha mikopo kwa wanufaika wa mikopo inayotolewa kupitia mradi wa SANVIN Viwanda, wameona kuna haja ya kupandisha kiwango cha mikopo kutoka Milioni 500 hadi kufikia Bilioni moja.
Ameyasema hayo Julai 18,2025 Mkuranga mkoani Pwani,katika kiwanda cha Amiron Medical Equipment Ltd, akiwa na wajumbe wa bodi hiyo katika hitimisho la ziara yao ya kutembelea wanufaika wa mradi huo ambayo iliyoanza Julai 15 2025 katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.
Prof. Kamuzora katika ziara hiyo akiwa na wajumbe wa bodi,ameonesha kufurahishwa na kuridhishwa utendaji wa mnufaika wa mradi wa SANVIN Viwanda,(Scheme) katika kiwanda cha uzalishaji wa vifaa tiba cha Amiron Medical Equipment ambapo amesema kuwa uwekezaji huo ni chachu ya mageuzi ya kiuchumi kwani itaongeza fursa ya ajira kwa vijana.
“Ni kitu kikubwa kimefanywa na SANVIN tunaona watanzania wenzetu wenye maono mazuri na ametueleza vizuri jinsi gani ambavyo amejipanga kuuza nje katika nchi za SADC” Profesa Kamuzora amesema.
Wakati huo huo,Profesa Kamuzora akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa bodi hiyo amesema wameameahidi kuwaita wadau wote wa mradi huo kuona namna bora ya kuwaunganisha sambamba na kuwezesha ushirikiano baina yao ili kuhuisha viwanda hivyo kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Amiron Medical Equipment Ltd, Bw. Monge Kigezo ameishukuru SANVIN kwa kuwawesha kufikia hatua hiyo kwani kupitia uwekezaji huo itapunguza matumizi ya fedha za kigeni ya manunuzi ya vifaa tiba vilivyokuwa vikinunuliwa nnje ya nchi.
“Tunashukuru kwa kweli bila SANVIN haya mafanikio yasingekuwepo, shukrani pekee kwakweli tunazitoa kwa Rais mama yetu Samia Suluhu Hassan kuweka mazingira wezeshi ya Viwanda binafsi lakini pia kutoa soko”Monge amesema.
Ziara hiyo imethibitisha kuwa uwezeshaji unaotolewa kupitia SANVIN Viwanda Scheme una mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko ya kweli kwa wajasiriamali wa ndani, huku NEEC ikiendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wake ili kufikia malengo ya maendeleo jumuishi na endelevu.
Mpaka sasa wanufaika wa Mradi wa SANVIN wamefikia 94 kutoka katika mikoa 13 ambayo ni pamoja na Arusha, Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya, Geita, Kilimanjaro, Pwani, Njombe, Dodoma, Iringa, Shinyanga, Rukwa na Singida.