• Tuzo inadhihirisha benki ya Stanbic kuongoza katika kuchochea uwekezaji, ajira, na ukuaji wa uchumi wa taifa.
• Tuzo hii inatambua mchango wa benki katika kuwezesha miradi inayochangia ukuaji wa uchumi wa kitaifa.
• Tuzo hii si tuzo ya ushindi tu, bali ni ushahidi halisi wa mchango wa benki katika uchumi wa Tanzania.
Dar es Salaam, Tanzania, Ijumaa 18 Julai 2025 – Benki ya Stanbic Tanzania imetangazwa kuwa Benki Bora ya Uwekezaji Tanzania katika Tuzo za Ubora Euromoney za 2025. Tuzo hii inatambua nafasi wa benki katika kutoa suluhisho za kimkakati za uwekezaji zinazounga mkono maendeleo ya taifa, kukuza viwanda vya ndani, na kuchangia ukuaji wa uchumi wa muda mrefu.
Tuzo hii inakuja wakati ambapo benki inaendelea kuwa mdau mkuu katika kuwezesha miradi yenye umuhimu mkubwa. Katika kipindi cha mwaka uliopita, Stanbic imeshiriki katika miamala iliyosaidia kupanua uwezo wa viwanda, kusaidia uwekezaji wa taasisi wa muda mrefu, na kukuza mazoea endelevu. Juhudi hizi zimesaidia kuzalisha ajira, kufungua fursa za kuuza bidhaa nje, na kuimarisha miundombinu ya kifedha nchini.
“Tuzo hii si kwa ajili ya kutambulika tu, bali kwa thamani tunayoileta kwa Taifa,” alisema Manzi Rwegasira, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic Tanzania. “Tumefanya kazi na wateja katika sekta ya umma na binafsi kuwezesha miradi inayobadilisha maisha na kukuza uchumi. Utambuzi huu ni ushahidi wa imani ya wateja wetu na uzito tunaoweka kwenye nafasi yetu kama mshirika wa uwekezaji.”
Timu ya benki, inayo hudumia uwekezaji na biashara, imesimamia miamala mingi ya kifedha yenye kuhitaji ujuzi mkubwa na wa kina wa masoko ya ndani na nje, kutathmini uhatarishi, na uwezo wa kubuni suluhisho zilizo muafaka. Hii ni pamoja na kupatiwa mitaji, mikopo ya muda mrefu, na huduma za ushauri zilizosaidia viwanda vya ndani, kuimarisha uendelevu kwenye uzalishaji, na kusaidia wawekezaji wa muda mrefu kulinda na kukuza fedha zao.
“Tumelenga kwenye miamala inayojenga uwezo na kuleta athari chanya ya muda mrefu,” alisema Ester Manase Lobore, Mkuu wa Idara ya Uwekezaji na Biashara. “Kuanzia kusaidia wateja kupanua uzalishaji hadi kusaidia taasisi zinazodhibiti akiba ya taifa kwa siku zijazo, lengo letu limekuwa kutoa thamani halisi. Tuzo hii inaakisi kazi kubwa isiyoonekana machoni pa wengi—lakini ndiyo inayosukuma ukuaji katika kila ngazi.”
Mbali na kuchakata uwekezaji, benki ya Stanbic pia imekuwa ikisaidia biashara za ndani kuunganishwa na fursa za kimataifa. Ikiungwa mkono na mtandao na utaalamu wa Standard Bank Group. Banki ya Stanbic imewezesha kampuni za Tanzania kufikia masoko ya kikanda, kusimamia fedha za biashara, na kujiandaa kwa uhamasishaji wa mitaji ya baadaye.
Sambamba na tuzo ya uwekezaji, Benki ya Stanbic pia imetangazwa kuwa Benki Bora Tanzania kwa Huduma kwa Wateja. Tuzo hii inaonesha dhamira ya benki kuweka mteja katikati ya mkakati wake, kuanzia kuboresha majukwaa ya kidijitali na kurekebisha huduma hadi kujenga uhusiano wa muda mrefu unaojengwa katika kuaminiana. Ni wazi kuwa kwa benki ya Stanbic, inaongoza si tu katika kujenga thamani ya kifedha, bali pia kutoa huduma thabiti inayojali watu binafsi.
Tuzo hizi zinaongeza mafanikio ya Standard Bank Group, ambayo imeshinda jumla ya tuzo 26 barani Afrika katika Tuzo za Euromoney za mwaka huu. Kundi hilo limetajwa kuwa Benki Bora Afrika, Benki Bora ya Uwekezaji Afrika, na Benki Bora kwa Makampuni Makubwa Afrika, miongoni mwa zingine, zikionesha rekodi imara ya utoaji thamani katika bara hili.
Benki ya Stanbic Tanzania imekuwa ikihudumu nchini kwa zaidi ya miaka 30, ikiunga mkono biashara za ndani, vipaumbele vya serikali, na ujumuishaji wa kifedha. Benki imekua na kuwa moja ya taasisi za kuaminika zaidi nchini, ikitoa huduma za kibenki kwa wawekezaji, huduma kwa watu binafsi, biashara, na ushauri wa kifedha.
“Tuzo hizi ni za kila mtu tunayemhudumia,” alisema Rwegasira. “Tutaendelea kusaidia ukuaji, kuleta suluhisho, na kuwa bega kwa bega na wateja wetu wanapojenga mustakabali wa nchi hii.”