Taasisi ya Youth Environmental Justice and Gender Equality (YOGE) kwa kushirikiana na Ona Stories wanatarajia kufanya Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ushiriki wa Kiraia kwa kutumia simulizi za Hadithi na Teknolojia Zinazochipukia ili kuhamasisha ushiriki wa wanawake na vijana katika nafasi za uongozi nchini Tanzania.
Mdahalo huo unatarajiwa kufanyika Julai 22, 2025 mkoani Morogoro, utawakutanisha viongozi 30 kutoka sekta mbalimbali zikiwemo siasa, biashara, dini, vyombo vya habari, sanaa na utamaduni kutoka mikoa mbali mbali ikiwemo ya Rukwa, Katavi, Dodoma, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam washiriki wakiwemo viongozi wanawake, wazee na vijana.
Katika kikao hicho, washiriki watapata fursa ya kutazama Filamu ya kumbukizi ya maisha na kazi za Bibi Titi Mohamed, mtetezi na kiongozi mwanamke aliyetoa mchango mkubwa katika kuhimiza ushiriki wa wanawake na vijana katika uongozi na nafasi za maamuzi nchini.
Filamu hiyo inalenga kuonesha mchango wake chanya na mkubwa katika kuchochea na kuhakikisha ushiriki endelevu wa wanawake na vijana katika nafasi za juu za uamuzi nchini.
Mdahalo huo unafanyika wakati muafaka hususani kufuatia uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 iliyozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alisisitiza kubuni mipango na sera zinazoshabihiana na utekelezaji wa dira hiyo kupitia vipaumbele mbali mbali vya kimkakati ikiwemo utawala ushiriki wa masuala ya kiraia, ujumuishaji na ushiriki wa wanawake, vijana na makundi maalum ili kuhakikisha tunatimiza lengo kuu la kubadilisha nchi yetu kuwa taifa la kipato cha juu, shirikishi na lenye maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2050.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mussa Kilakala, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kikao hicho.