Na John Bukuku
Dar es Salaam, 21 Julai, 2025
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha maandalizi ya uchaguzi yanafanyika kwa kuzingatia misingi ya sheria, maadili, na utulivu ili kuepusha malalamiko kutoka kwa wadau wa uchaguzi.
Akizungumza leo katika ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa waratibu wa uchaguzi, wasimamizi na maafisa kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, Mjumbe wa Tume hiyo, Balozi Omar Ramadhan Mapuri, amesisitiza kuwa utekelezaji wa majukumu ya uchaguzi unapaswa kuongozwa na Katiba, sheria, kanuni na miongozo ya Tume.
“Tunahitaji uchaguzi wenye amani, utulivu na unaoendeshwa kwa weledi wa hali ya juu. Hili linawezekana kama kila mmoja atasoma kwa kina na kuelewa nyaraka zote muhimu za uchaguzi, na kuuliza maswali pale panapotokea changamoto za uelewa,” alisema Balozi Mapuri.
Katika hatua nyingine, Balozi Mapuri amewataka wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha wanatambua mapema vituo vya kupigia kura ili kupanga mahitaji mahsusi na kuhakikisha kuwa siku ya kupiga kura haina vurugu wala mkanganyiko.
Ameonya pia kuhusu tabia ya upendeleo katika uteuzi wa watendaji wa vituo vya kupigia kura, akisisitiza kuwa waajiriwe watu wenye sifa zinazostahili kama vile weledi, uzalendo, maadili na bidii ya kazi. “Tusiingize ndugu na jamaa wasio na sifa. Uchaguzi ni suala nyeti linalohitaji uadilifu wa hali ya juu,” alionya.
Mafunzo hayo yamejumuisha washiriki 106 na yanatarajiwa kumalizika Julai 23, 2025, yakilenga kuwajengea uwezo waratibu wa uchaguzi wa ngazi ya jimbo pamoja na wasimamizi na wasaidizi wa uchaguzi ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa mujibu wa sheria.