21 Julai, 2025, Bagamoyo, Pwani
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt. Dkt. Hussein Mohamed Omar ametembelea Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu-ADEM kuona utekelezaji wa shughuli zinazotekelezwa na Wakala.
Dkt Hussein amefanya ziara hiyo ikiwa ni mara yake ya kwanza kufika ADEM tangu alipoteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu mnamo mwezi Juni, 2025.
NAIBU Katibu Mkuu huyo, amesema lengo la ziara hiyo ni kuifahamu ADEM na kuona shughuli zinazotekelezwa na ADEM ambapo ametumia fursa hiyo kuipongeza Menejimenti ya ADEM kwa utekelezaji wa majukumu ya Wakala kwa ufanisi hususani mafunzo ya uongozi na usimamizi wa elimu yanayolenga kuwajengea umahiri viongozi katika sekta ya elimu kuhusu uongozi na usimamisi wa elimu.
Dkt. Hussein pia amesisitiza Menejimenti ya ADEM kuongeza nguvu katika kufanya tafiti kuhusu mahitaji ya mafunzo ya uongozi na usimamizi wa elimu kwenye shule za Serikali na zile za binafsi yanayolenga usimamizi thabiti wa elimu ya Amali ili kuisaidia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknokojia kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la 2023 inayosisitiza utekelezaji wa elimu ya kujitegemea nchini.
“Nimesikia utekelezaji wa shughuli mnazozitekeleza kama Wakala, nawapongeza sana, lakini natoa rai kwa uongozi wa Wakala, jiimarisheni katika kufanya tafiti zinazoendana na muktadha wa usimamizi wa elimu ya Amali inayosisitizwa kwenye Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la 2023 ili Wakala uishauri Wizara ya Elimu kuhusu namna bora ya kusimamia eneo la elimu ya Amali, hivyo kuisaidia Wizara kufikia malengo yake katika utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo iliyofanyiwa maboresho.” Amesema Dkt Hussein.
Nae Mtendaji Mkuu wa ADEM Dkt. Maulid J. Maulid akielezea utekelezaji wa shughuli za Wakala kwa Naibu Katibu Mkuu Dkt Hussein amesema ADEM imeendelea kutoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi ya Uongozi, Usimamizi na Uthibiti Ubora wa Elimu, kufanya tafiti na kutoa machapisho mbalimbali na kutanabaisha kuwa Wakala pia umejiimarisha katika utoaji wa mafunzo hayo kwa kuanzisha ushirikiano na Taasisi za kimataifa kama vile VVOB-Education for Development na International Institute for Educational Planning – UNESCO.
Aidha, Dkt. Maulid, pia ametumia fursa hiyo kuishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Mashirika ya Kimataifa kama vile World Bank kupitia miradi mbalimbali ya elimu kwa namna wanavyounga mkono utekelezaji wa shughuli za ADEM.
Katika ziara hiyo, Dkt. Hussein aliambatana na Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bw. Sebastian Innosh.