Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi, amesema kuwa Tanzania ipo tayari kwa ajili ya kuandaa Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), yatakayoanza rasmi Agosti 2, 2025.
Akizungumza mara baada ya ziara ya ukaguzi wa miundombinu ya michezo jijini Dar es Salaam, Dkt. Yonazi alisema maandalizi yamefikia hatua nzuri na viwanja viko tayari kwa mashindano hayo makubwa.
Akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Makatibu Wakuu ya CHAN na AFCON, Dkt. Yonazi alitembelea viwanja vya Benjamin Mkapa, Isamuhyo, Shule ya Sheria na Gymkhana, akisisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha miundombinu yote inakidhi viwango vya kimataifa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa, ametoa wito kwa Watanzania kuonesha uzalendo kwa kujitokeza kwa wingi viwanjani kuishangilia Taifa Stars.