Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza DCP Wilibroad Mutafungwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo pichani)
…………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Jeshi la polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kuiba samaki wanaofugwa kwenye vizimba vya kufugia samaki vilivyopo katika mialo ya Nyambilo, Kongoro,Chabula na Kitongosima wilayani Magu.
Akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Mwanza leo Julai 21,2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Wilbroad Mutafungwa amesema 18 Julai, 2025 majira ya saa kumi na mbili jioni jeshi hilo kupitia askari wa kikosi cha wanamaji na askari wengine wameendelea kufanya doria katika ziwa Victoria kwa lengo la kudhibiti matukio ya wizi wa samaki yanayofanywa na wavuvi wasiokuwa waaminifu.
“Kikosi hicho kilifanikiwa kuwakamata Elikana Jeremiah (47) mfanyabiashara wa samaki na mkazi wa Mwabui Nyanguge,Samba Mwambala (41) mkazi wa Mahina Nyakato Wilaya ya Nyamagana,Mganga Kabere (49) mvuvi mkazi wa Nyambiro Nyanguge amekamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na wizi wa samaki kwenye vizimba na kuwauza kwenye masoko,Kapili Nzali (21) mvuvi mkazi wa Mwamayombo Nyanguge amekamtwa kwa tuhuma za wizi wa samaki kwenye vizimba pamoja na Joseph Pagwa (61) mvuvi na mkazi wa Kijiji cha Lutale*,
Amesema DCP Mutafungwa pamoja na kukamatwa kwa watuhumiwa hao pia vimekamatwa vielelezo ambavyo ni samaki 89 aina ya sato,jokofu moja la kuhifadhia samaki na mtumbwi mmoja wenye namba za usajili TZ MUM 6943.
Aidha, watuhumiwa hao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiiba samaki hao kwa madai kuwa ni wa kwao hivyo wale wa vizimba ni kama wamevamia ziwa.
“Tunapenda ieleweke kwamba uvuvi unaruhusiwa kwa mujibu wa sheria hata wawekezaji wa vizimba na wenyewe wanaruhusiwa kuendesha shughuli hizo pasi na kuvunja sheria za nchi na nilazima na wajibu wa jeshi la polisi kuhakikisha hakuna mvuvi anayemwibia mvuvi mwingine,” amesema DCP Mutafungwa.