Na WMJJWM- Karatu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu amewahimiza wananchi wilayani Karatu mkoani Arusha kuchangamkia fursa ya Mikopo inayotolewa na Benki ya NMB ili kukuza biashara zao.
Dkt Jingu ametoa wito huo leo 22 Julai 2025 wakati akihutubia mkutano wa kuwafahamisha fursa zinazotolewa na Serikali na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Wilayani humo.
“Ujumbe wangu kwenu ni kwamba, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, imeweka mazingira rafiki kwa wafanya biashara ndogondogo kupata mikopo ya aina mbalimbali ili mueweze kuendesha shughuli zenu za kiuchumi kwa maendeleo yenu na Taifa” amesema Dkt Jingu.
Dkt Jingu ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuchangamkia fursa ya kushindania fursa ya manunuzi ya serikali ya asilimia 30 ambayo inatolewa na taasisi zote za Serikali.
Baada ya marekebisho ya sheria ya ununuzi wa umma mwaka 2023, sasa wananchi mnaweza kujiunga katika vikundi mkiwa na biashara au huduma fulani, mnaweza kupata tenda za Serikali ambazo zinapatikana katika Halmashauri zote nchini.
Naye Katibu Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu Juma Hokonoro amesema kuna fursa mbalimbali za kiuchumi zikiwemo za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanayoendesha mafunzo ya kilimo na ufugaji hivyo ni muhimu wananchi wakazichangamkia kwa lengo la kuongeza kipato na kukuza uchumi wao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika Lisilo la Kiserikali la Food for His Children Honorina Honorata amesema kupitia Shirika hilo wataendelea kutoa mafunzo ya ufugaji na kilimo kwa wananchi ikiwa ni sehemu ya kuwezesha jamii kuondokana na umaskini.