Na Fauzia Mussa
WAZIRI wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Zanzibar, Shamata Shame Khamis, amesema maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Mkulima (Nane Nane) yamekamilika, ambapo maonesho hayo yanatarajiwa kufunguliwa rasmi Agosti 2 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukagua viwanja vya maonesho vilivyopo Dole Kizimbani, Wilaya ya Magharibi ‘A’, Mkoa wa Mjini Magharibi, Waziri Shamata alisema maonesho ya mwaka huu yanalenga kuhamasisha wakulima kulima kwa ubunifu, kuongeza tija, na kutumia teknolojia za kisasa katika kilimo.
“Wizara imeandaa maonesho haya kwa dhamira ya kuimarisha kilimo kwa kutumia zana za kisasa, kukuza kilimo hai, na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu faida za kilimo bora,” alisema Waziri Shamata.
Alieleza kuwa maonesho hayo ni sehemu ya mpango wa Serikali katika kuendeleza kilimo biashara, kupunguza utegemezi wa chakula kutoka nje ya nchi, pamoja na kuwawezesha vijana kushiriki katika kilimo cha kisasa, hususan kilimo cha umwagiliaji.
Waziri huyo aliongeza kuwa Serikali inalenga kuimarisha uzalishaji wa mazao ya viungo, mboga mboga, matunda, mizizi, nazi na karafuu sambamba na kutoa huduma bora za mifugo na kusimamia rasilimali za misitu kwa lengo la kuhifadhi mazingira.
Kwa mujibu wa Waziri Shamata, kaulimbiu ya mwaka huu ni “Kilimo ni utajiri, Tunza Amani, Tulime Kibunifu”, ambapo lengo ni kuhamasisha wakulima kutumia mbinu bora za kilimo, kukuza pato lao binafsi na la taifa, na kuhimiza utunzaji wa amani ambayo ni msingi wa maendeleo.
Alibainisha kuwa maonesho ya mwaka huu yatakuwa ya aina yake kutokana na ongezeko kubwa la washiriki na hadi sasa, wajasiriamali 222, washiriki binafsi 311, taasisi za serikali 49, na mashirika binafsi 40 wamethibitisha kushiriki.
“Ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao wakati wa maonesho hayo umeimarishwa kikamilifu,” aliongeza.
Waziri alihitimisha kwa kusema kuwa Wizara yake imejipanga kuhakikisha maonesho ya mwaka huu yanafana zaidi ya yaliyopita, na kutoa fursa kwa wananchi, wakulima, na wawekezaji kupata elimu, teknolojia na mbinu mpya za kisasa katika kilimo na ufugaji.