
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) – Taaluma, Profesa Emmanuel Balandya (katikati) akimkabidhi zawadi Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Anne Sophie Avé wakati alipotembelea Chuo hicho leo Julia 23, 2025 jijini Dar es Salaam.

Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Profesa Emmanuel Balandya akizungumza na wanafunzi na wafanyakazi wa MUHAS katika mkutano ulioandaliwa na Kitengo cha Kimataifa na Mahafali cha MUHAS wakati Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Anne Sophie Avé alipotembelea Chuo hicho leo Julia 23, 2025 jijini Dar es Salaam.


Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Anne Sophie Avé akizungumza na wanafunzi na wafanyakazi wa MUHAS wakati alipotembelea Chuo hicho.

Mkuu wa Kitendo cha Internationalization and Convocation Unit MUHAS Dkt. Maryam Amour akizungumza na wanafunzi na wafanyakazi wa MUHAS wakati Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Anne Sophie Avé alipotembelea Chuo hicho.






……..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Tanzania kupitia Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Bordeaux kutoka nchini Ufaransa, zimeahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu katika sekta ya afya, kwa kuweka mkazo katika kuimarisha ushirikiano wa kielimu katika tiba na utafiti, ili kukabiliana na changamoto za afya duniani.
Akizungumza leo Julai 23, 2025, jijini Dar es Salaam, wakati Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Anne Sophie Avé, alipotembelea Chuo Kikuu cha MUHAS, Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Profesa Emmanuel Balandya, amesema kuwa ushirikiano huo unalenga kubadilishana uzoefu kati ya Tanzania na Ufaransa ili kuboresha utoaji wa elimu ya afya.
Profesa Balandya amesema kuwa mahusiano kati ya taasisi hizo ni mazuri, na kwamba wako tayari kuyaendeleza ili kuleta tija katika maeneo mbalimbali ya elimu chuoni hapo.
“Ushirikiano huu utasaidia wanafunzi wa MUHAS kwenda Ufaransa kupata mafunzo, na pia wanafunzi na walimu kutoka Ufaransa kuja kufundisha hapa chuoni,” alisema Profesa Balandya.
Akizungumza na wanafunzi na wafanyakazi wa MUHAS katika mkutano ulioandaliwa na Kitengo cha Kimataifa na Mahafali cha MUHAS, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Anne Sophie Avé, amesisitiza umuhimu wa kutumia nguvu za taasisi na maarifa ya pamoja kushughulikia changamoto za afya duniani.
“Tunataka kukuza ushirikiano kati ya vyuo vikuu katika maeneo mbalimbali, hususan sekta ya afya. Tuna mengi ya kujifunza kutoka kwa nchi kama Tanzania,” amesema Balozi Anne Sophie Avé.
Ameongeza: “Kwa kufanya kazi nanyi, tunajifunza kuhusu magonjwa ambayo sisi hatuyafahamu vizuri. Mafunzo ya pande zote mbili yatasaidia kukabiliana na changamoto za kiafya katika dunia hii inayobadilika.”
Hata hivyo, Balozi huyo amesisitiza pia umuhimu wa kuwekeza kwa vijana, huku akipongeza juhudi zinazofanywa na MUHAS katika kuzalisha wataalamu mahiri na bingwa katika sekta ya afya.
“Tunaamini vijana ndiyo taifa la kesho, hivyo kuwekeza kwa vijana ni kuwekeza kwa siku zijazo,” alisema Balozi huyo.