Benki ya Dunia (WB) imeeleza kuwa itatoa fedha za utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo mkubwa wa kilovolti 400 kutoka nchini Uganda hadi Tanzania.
Hayo, yameelezwa na Mtaalam wa Nishati kutoka Ofisi ya Benki ya Dunia nchini Tanzania, Dkt. Rhonda Jordan wakati alipofanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mha. Felchesmi Mramba katika Ofisi za Wizara ya Nishati Mji wa Serikali Mtumba Julai, 23 Jijini Dodoma.
Dkt. Rhonda amesema kuwa kwa sasa benki hiyo imeridhia kutekeleza mradi huo baada ya kujiridhisha kuwa hauna athari za kimazingira kama ilivyokuwa ikielezwa hapo awali.
“Bodi ya Wakurugenzi sasa itapitisha fedha kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi huo, ambao ulikuwa ukisuasua kutekelezwa kwa madai ya kuathiri mazingira, lakini sasa bodi imeridhika na itatoa fedha za kuanza kuutekeleza”, amesema Dkt. Rhonda
Katika hatua nyingine, Dkt. Rhonda ameialika Wizara ya Nishati kushiriki katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika Jijini New York nchini Marekani mwezi Semptemba, 2025.
Katika mazungumzo yao, Katibu Mkuu Mramba amemueleza Dkt.Rhonda kuwa wataendelea kushirikiana na Benki ya Dunia katika miradi mbalimbali ya Nishati ikiwemo ule wa usafirishaji umeme wa Tanzania-Zambia (TAZA) na mingine inayofafana kama hiyo.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mha. Innocent Luoga na Mhandisi Nishati Mkuu John Mageni.