Maofisa na wapiganaji wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) Zanzibar wamepatiwa mafunzo JKU YAKATIWA MAFUNZO YA UMILIKI NYUMBA ZA KISASA KUPITIA MIKOPO NAFUU YA PSHS kuhusu umiliki wa nyumba za kisasa kupitia mpango wa Public Servants Housing Scheme (PSHS), unaoratibiwa na Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC).
Mafunzo hayo, yaliyofanyika katika Makao Makuu ya JKU Saateni, yakilenga kuwapa uelewa wa kina watumishi wa jeshi hilo kuhusu fursa ya kumiliki makazi bora kwa njia ya mikopo nafuu yenye masharti rafiki, inayokatwa moja kwa moja kutoka kwenye mishahara yao.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa ZHC, Sultan Said Suleiman, alieleza kuwa mpango wa PSHS umebuniwa mahsusi kwa ajili ya kuwawezesha watumishi wa umma kumiliki nyumba bora kupitia mikopo ya muda mrefu, kuanzia miaka 10 hadi 25, kwa riba nafuu ya tarakimu moja (single digit), pamoja na bima ya maisha inayowalinda wanufaika dhidi ya majanga mbalimbali ikiwemo vifo.
“Mpango huu unaleta unafuu mkubwa kwa wanunuzi wa nyumba na pia ni chachu ya kuimarisha maendeleo ya miji, kupunguza ujenzi holela na hatimaye kuijenga Zanzibar mpya yenye mipango bora ya makazi na ustawi wa jamii nzima,” alisema Sultan.
Alibainisha kuwa baadhi ya miradi inayopatikana kupitia mpango huo ni pamoja na Mombasa kwa Mchina Phase II, Mwinyi Housing Scheme – Kisakasaka, na mradi wa Chumbuni, yote ikiwa imejengwa kwa viwango vya kisasa na ubora wa kimataifa.
Kwa upande wake, Kamanda wa JKU, Col. Makame Abdalla Daima, aliwataka maofisa na wapiganaji wa jeshi hilo, hasa vijana, kuchangamkia fursa hiyo mapema ili kujihakikishia umiliki wa nyumba bora kwa ajili ya familia zao.
“Fursa hii ni uwekezaji wa maisha. Serikali imeweka mazingira rafiki kwa kila mtumishi kumiliki nyumba bila kikwazo cha masharti magumu kutoka taasisi za fedha. Msiiache ipite,” alisisitiza Kamanda Col. Daima.
Pia, Kamanda huyo alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa dira yake thabiti ya kujenga Zanzibar mpya yenye usawa katika upatikanaji wa huduma za msingi kwa wananchi wote.
Katika mafunzo hayo, maofisa wa mauzo na masoko kutoka ZHC waliwasilisha kwa undani taarifa za miradi ya nyumba, gharama zake, pamoja na taratibu za kujiunga na vigezo vya kuhitimu kupatiwa mikopo hiyo.
Mpango wa PSHS unaelezwa kuwa sehemu ya mkakati wa Serikali wa kufanikisha malengo ya kitaifa ya kuhakikisha kila mtumishi wa umma anapata makazi salama, bora na yanayokidhi mahitaji ya kijamii na kiuchumi ya karne ya 21.