Na WAF, Arusha
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, ametoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuzingatia ushauri na maelekezo ya wataalam wa afya na malezi ili kuwalea watoto, kwa kuweka mkazo maalum wa lishe bora, malezi yenye upendo na mazingira salama kwa ajili ya ustawi wao, kwakuwa watoto ni hazina ya taifa la kesho.
Dkt. Shekalaghe ametoa wito huo Julai 23, 2025, mkoani Arusha, wakati akifungua Kongamano la pili la Kitaifa la Afya na Ustawi wa Watoto, ambapo amesisitiza kuwa taifa haliwezi kuwa na viongozi bora wa baadaye ikiwa jamii haitawalea watoto kwenye misingi imara ya afya, elimu na maadili.
“Watoto wasipo pata malezi vizuri, wakakosa lishe bora, mazingira salama na malezi yanayojali maendeleo yao ya kimwili na kiakili, hatuwezi kuwa na viongozi bora wa kesho, rai yangu ni muhimu jamii kutambua na malezi bora hujengwa kwa kuzingatia ushauri wa wataalam wa afya na wataalam wa malezi,” amesema Dkt. Shekalaghe.
Ameongeza kuwa familia zinapaswa kuzingatia kila nyanja ya afya ya mtoto kuanzia mlo anaopata, mazungumzo ya kila siku, michezo anayoshiriki, hadi mazingira anayoishi.
“Afya siyo tu kukosekana kwa ugonjwa, bali ni hali njema kimwili, kiakili, kijamii na kiutamaduni. Kwa hiyo, tuwalee watoto wetu kwa njia sahihi ili wajenge taifa lenye msingi thabiti,” amesisitiza.
Dkt. Shekalaghe pia amewahimiza wataalam na watoa huduma za afya nchini, hususan wale wanaohudumia watoto, kulenga zaidi kuzuia vifo na kujikita pia kwenye kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora na malezi chanya kwa watoto.
Kwa upande wake, Rais Mteule wa Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania, Dkt. Theopista Jacob, amesema kuwa, licha ya uwekezaji mkubwa na juhudi za Serikali za kuhakikisha watoto wanapata huduma za chanjo, bado ipo haja ya Idara ya Huduma za Chanjo (IVD) kushirikiana kwa karibu na watumishi wa afya ili kila mtoa huduma awe na uelewa sahihi na anasaidia kupata taarifa kwa wakati kuhusu watoto wanaopata magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.
Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kufanikisha juhudi za kudhibiti na kuzuia magonjwa yanayoweza kutokomezwa kwa njia ya chanjo.