Na Silivia Amandius
Kagera
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mheshimiwa Erasto Sima, amezindua rasmi Mradi wa Lishe Shuleni unaotekelezwa kwa ushirikiano na shirika la kimataifa la Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN), ukilenga kuboresha lishe ya wanafunzi katika mikoa ya Kagera.
Uzinduzi huo umefanyika Juni 23, 2025 katika Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, ambapo viongozi wa serikali, wadau wa maendeleo na wawakilishi wa mashirika walihudhuria.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mh. Sima alisema licha ya Mkoa wa Kagera kuwa miongoni mwa mikoa yenye uzalishaji mkubwa wa chakula, bado changamoto ya lishe duni kwa watoto ipo. Alipongeza GAIN kwa kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha watoto wa shule wanapata lishe bora.
“Suala la lishe limekuwa changamoto kubwa, licha ya rasilimali tulizonazo. Mradi huu utasaidia kubadili hali hiyo kwa vitendo, hasa mashuleni,” alieleza DC Sima.
Kwa upande wake, Meneja Mradi wa Urutubishaji kutoka GAIN, Bw. Archard Ngemela, alifafanua kuwa mradi huu ni wa majaribio na utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 12 kwa gharama ya dola za Kimarekani 145,000 (sawa na shilingi milioni 374.3). Mradi unahusisha shule 54 kutoka wilaya za Bukoba, Muleba na Misenyi, na unalenga wanafunzi 34,200.
Mradi huu utahusisha kilimo cha mazao yenye virutubisho vingi ikiwemo maharage, mahindi lishe na mboga mboga, ambavyo vitapandwa katika mashamba ya shule husika kama njia ya kuhakikisha upatikanaji wa chakula chenye virutubisho vya kutosha.
Afisa Lishe wa Mkoa wa Kagera, Bi. Joanitha Jovin, alibainisha kuwa shule 18 za msingi na sekondari kutoka kata sita za Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba — Kasharu, Kyamulaile, Ruhunga, Kaagya, Rubale na Rukoma — zitanufaika na mradi huo.
Bi. Joanitha alieleza kuwa mkoa wa Kagera umechaguliwa kwa sababu ya hali duni ya lishe kwa baadhi ya maeneo, hali nzuri ya hewa, upatikanaji wa mbegu bora na uhusiano mzuri wa muda mrefu kati ya mkoa huo na GAIN.
Mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Masuala ya Lishe pamoja na Muongozo wa Ulaji Bora wa Chakula Shuleni wa mwaka 2020.