

Ili kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo 2034 kama ilivyoanishwa katika Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na Halmashauri ya Manyoni wametoa majiko ya gesi zaidi ya 500 ya Kilogramu 6 kwa wananchi wa Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.
Akizungumza wakati wa kukabidhi majiko hayo kwa wananchi, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi ametoa rai kwa wananchi kuunga mkono kampeni hiyo ya Nishati Safi ya Kupikia ili kuendelea kutunza mazingira.
“Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa ni kinara wa kampeni hii ya nishati safi ya kupikia Duniani. Sisi kama wananchi hatuna budi kumuunga mkono kwa kuhakikisha tunatumia nishati safi ya kupikia ili kutunza mazingira yetu kwa kizazi cha sasa na hata kizazi kijacho ili ile sifa ya Tanzania ya kijani iendelee kwa vizazi vyote,” amesema Ussi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Mhe. Dkt. Vincent Mashinji amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni imejipanga kuendelea kutekeleza kampeni hiyo ya nishati safi ya kupikia kwa kutenga fedha za mapato ya ndani kuwapatia wananchi nishati safi za kupikia pamoja na kujenga miundombinu ya nishati safi ya kupikia katika shule na taasisi zingine za serikali katika Wilaya hiyo.
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea na ugawaji wa majiko ya gesi ya Kilogramu 6 kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50 kwa wananchi wa Mkoa wa Singida, ambapo majiko ya gesi 19,530 yamepangwa na yanaendelea kugaiwa kwa wananchi katika Mkoa huo huku Wilaya ya Manyoni ikiwa imetengewa majiko ya gesi 3,255.