Kamishna Mkuu wa TRA, CPA Yusufu Juma Mwenda (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno na wakionesha hati ya makubaliano ya ushirikiano mara baada ya kusaini makubaliano ya upatikanaji wa taarifa mbalimbali zikiwemo za kikodi na kihesabu ikiwa sambamba na kusomana kwa mifumo kati ya taasisi hizo mbili.

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano wa miaka mitano na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) ili kuendelea kuboresha huduma kwa walipa kodi.
Akizungumza leo Julai 25,2025 wakati wa hafla ya utiaji saini, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, alisema lengo kuu la makubaliano hayo ni kubadilishana taarifa kati ya taasisi hizo mbili kwa lengo la kuimarisha mfumo wa ukusanyaji kodi.
“Si kwamba mashirikiano kati yetu hayakuwepo yapo na yanaendelea kuwepo. Ndiyo maana leo tunayaweka rasmi kwenye maandishi ili mifumo yetu isomeane. Hii itaiwezesha TRA kufanya maamuzi sahihi katika ukadiliaji wa kodi na kupunguza migogoro kati ya mamlaka na walipa kodi,” amesema Mwenda.
Ameongeza kuwa NBAA itasaidia kuimarisha juhudi za pamoja katika kuwaelimisha na kuwawezesha wataalamu wa kodi, wahasibu, wakaguzi wa hesabu, wanafunzi wa fani ya uhasibu, pamoja na wadau wengine kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kwa kuzingatia maadili ya taaluma, hivyo kuondoa tuhuma dhidi yao.
Mwenda amesema ushirikiano huo ni utekelezaji wa maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, dk Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha taasisi za umma zinafanya kazi kwa kushirikiana.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa NBAA,Pius Maneno, amesema kuwa hivi karibuni NBAA imezindua mfumo mpya uitwao NBAAVN, ambao utarahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi za hesabu kwa wadau mbalimbali na kupambana na changamoto ya uwepo wa wahasibu vishoka kwani kupitia mfumo huo, taarifa zote za hesabu zitapewa namba maalum za utambuzi.
“Makubaliano haya hayatakuwa tu ya miaka mitano kama ilivyoandikwa, bali ni mwendelezo wa kuboresha huduma kwa walipa kodi, kuondoa malalamiko, na kuhakikisha kuwa Taifa linapata kodi stahiki kwa maendeleo endelevu,” amesema Maneno.
Makubaliano hayo ni ya pili kusainiwa na NBAA kwa mwaka 2025, baada ya kusaini makubaliano mengine na Taasisi ya Wahasibu, Wakaguzi na Washauri wa Kodi Zanzibar (ZIAAT) Mei 16, kwa lengo la kuimarisha taaluma ya uhasibu na ushauri wa kodi katika pande zote mbili za Muungano.