NA DENIS MLOWE,IRINGA
Mkuu wa wilaya ya Kilolo, Astomini Kyando amepongeza maonyesho ya Ajira kwa Vijana ya 2025 yaliyoandaliwa na Taasisi ya Swiss Contact kupitia mradi wa Skills For Employment Tanzania na kufadhiliwa na Ubalozi wa Uswisi kuwa ni mkombozi kwa vijana kutokana na maudhui yake.
Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Maonyesho hayo kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Iringa, Kheri James, DC Kyando alisema kuwa maonyesho hayo yameweza kuongeza uelewa wa vijana kuhusu ujuzi unaohitajika katika soko la ajira kwa kuwawezesha waajiri na watoa mafunzo ya ujuzi kuzungumzia mwelekeo wa sekta mbalimbali na mabadiliko ya ujuzi yanayohitajika sokoni.
Alisema kuwa maonyesho hayo yameweza kutoa nafasi kwa vijana kushiriki katika majadiliano ya wazi na ya kijamii ambapo watakutana moja kwa moja na wanawake na wanaume waliopata mafanikio katika biashara, waajiri na wataalamu, kuuliza maswali na kujenga mahusiano ya kikazi.
Aidha amepongeza maonyesho hayo kuwa yamefanikiwa kuwapa vijana mazingira rafiki ya kupata maarifa kuhusu maandalizi ya ajira na namna ya kushirikiana na waajiri pamoja na taasisi za kifedha kwa ajili ya kupata msaada wa kifedha.
“Maonesho haya si tu nafasi ya kupata maarifa, bali ni hatua ya kuanza safari ya mafanikio. Vijana wa Iringa, chukueni hatua, tambueni uwezo wenu, fanyeni maamuzi yenye mwelekeo wa maendeleo. Tunawashukuru wadau wetu wa Uswisi kwa kuona thamani ya vijana wetu.” Alisema
Vile vile aliongeza kuwa ubalozi wa Uswisi unahitaji kupongezwa kwa kuweza kufadhili na kutangaza na kuonyesha mchango wa mradi wa SET, ikiwa ni sehemu ya kuonyesha ushiriki wa Uswisi na Swiss contact katika kukuza maendeleo ya ujuzi nchini Tanzania.
Alisema kuwa Maonyesho hayo ya Ajira kwa Vijana yanayofanyika katika Uwanja wa Mwembetogwa yameweza kuwafikia vijana wengi ambao ni zaidi ya 3000 hadi sasa yanahitajika kuwa endelevu kwa kuwa yameonyesha manufaa zaidi huku zaidi ya washirika na wadau 50 wakiwemo waajiri, watoa mafunzo ya ujuzi, taasisi za serikali, asasi zisizo za kiserikali (NGOs), taasisi za kifedha, na wengine waliokuwa wakionesha huduma na fursa zao katika maonyesho haya yenye kauli mbiu Kijana: Ujuzi Wako, Fani Yako, Chaguo Lako yana tija kwa mkoa na Taifa kwa Ujumla.
Kwa upande wake Balozi Nicole Providoli alisisitiza dhamira ya Uswisi katika kusaidia maendeleo ya vijana ni nguvu kazi ya taifa na chachu ya maendeleo na kuongeza kuwa upitia maonesho haya na mradi wa SET, tunalenga kuwajengea vijana uwezo wa kuchukua nafasi zao kikamilifu katika jamii na uchumi na kujivunia kushirikiana na Iringa kuwa mfano wa mafanikio.
Naye Rudolf Nuetzi, Mkurugenzi wa Swisscontact nchini Tanzania, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano endelevu kati ya wadau kwa kupitia mradi wa SET, Swisscontact inaendeleza juhudi za kuwaunganisha vijana na fursa za kazi na ujasiriamali hivyo ni jukwaa la kuwaleta pamoja waajiri, watoa mafunzo, serikali, na vijana ili kujenga mfumo unaozalisha ajira na maendeleo.




