Na Mwandishi Wetu
Waziri Mkuu mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndg. Mizengo Pinda, amesema ushirikiano na mshikamano wa vyama sita rafiki vya ukombozi Afrika unapaswa kudumishwa kwa kuzingatia maadili ya ukombozi, misingi ya haki, usawa wa maendeleo jumuishi kwa wananchi kwa kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo Ajenda 2063 ya Afrika Tuitakayo.
Pinda aliyasema hayo akimwakilisha Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano Mkuu Maalum wa Vyama sita rafiki vya ukombozi Kusini mwa Afrika mjini Gauten, Afrika Kusini. Vyama hivyo sita ni pamoja na ANC (Afrika Kusini), MPLA (Angola), SWAPO (Namibia), ZANU PF (Zimbabwe), FRELIMO (Msumbiji) na Chama Cha Mapinduzi.
Katika mkutano huo ulioanza Julai 25 na unatarajia kumalizika Julai 28, dhima kuu ni kutetea mafanikio ya ukombozi, kusukuma maendeleo jumuishi ya kijamii na kiuchumi, na kuimarisha mshikamano kwaajili ya Afrika bora. Pinda alisema, mustakabali wa mataifa ya Tanzania, Afrika Kusini, Msumbiji, Zimbabwe, Angola na Namibia unategemea kwa kiasi kikubwa uhusiano wa karibu kati ya viongozi na wananchi wake.
Akitoa salamu za CCM kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM, Pinda alisema vyama rafiki vinawajibika kuhakikisha kuwa vinadumisha mshikamano, maadili ya ukombozi, na misingi ya haki, usawa na maendeleo jumuishi kwa wananchi wote kama ishara ya kutekeleza kwa vitendo Ajenda 2063 ya Afrika tuitakayo, kwa kuwa vimebeba dhima kubwa ya maendeleo.
Alisema umuhimu wa kuwajumuisha vijana katika kila hatua ya harakati za kisiasa na maendeleo ya jamii ni njia muhimu ya kujenga kizazi cha vijana wazalendo, wenye ufahamu wa historia ya vyama hivyo kama ilivyokuwa kwa waasisi wa vyama hivyo ambao walisimama mstari wa mbele katika kujenga vyama hivyo pamoja na kuleta amani kwa mataifa yao.
“Tutakapokuwa na jamii yenye utambuzi wa mchango wa waasisi wa Afrika kama akina Julius Nyerere, Kwame Nkurumah, Nelson Mandela, Sam Nujuma na wengineo kadhalika. Maendeleo ya Afrika yatakuja kwa dhamira ya dhati ya kulinda, kudumisha na kuendeleza misingi ya waasisi wetu ikiwa vijana watakuwa sehemu ya maendeleo hayo.” alisema
Alisema mkutano huo ni muhimu katika kuwaleta viongozi pamoja na ametoa rai kuhakikisha wanautumia mkutano huo kujenga fikra za vijana kwa ajili ya kuendeleza mambo mazuri yaliyoasisiwa na waasisi kwa kuwa vijana pamoja na kuviboresha vyama hivyo viendelee kuwa chachu ya mabadiliko kwa kizazi cha sasa na cha baadae.
Katika hatua nyingine, Pinda pia alishiriki shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na ufunguzi rasmi wa mkutano wa vyama rafiki vya ukombozi pamoja na kushiriki kikao maalumu cha ujumbe wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), ambapo mijadala ya kimkakati kuhusu mwelekeo wa kisiasa na kijamii wa vyama vya ukombozi katika kizazi kipya cha uongozi barani Afrika ilijadiliwa.