Â
👉Sera ya Maudhui ya ndani ikitumika katika sekta zote itachochea ukuaji wa uchumi wa nchi kwa haraka
Serikali ya Tanzania na nchini kwa ujumla imeanza kunufaika na sekta ya madini ambapo uchangiaji wake katika Pato la Taifa (GDP) unazidi kukua siku hadi siku ambapo takwimu za Wizara ya Madini zinabainisha kuwa mchango wake umefikia asilimia 9.
Mafaniko haya yanatokana na Serikali kuweka sheria na sera madhubuti ambazo zinasimamia uendeshaji wa shughuli za uchimbaji wa madini nchini ambazo ni rafiki kwa wawekezaji pia zinalenga kunufaisha taifa na wananchi.
Moja ya sera ambayo inaonekana kuwa imelenga kunufaisha wananchi wazawa kutokana na rasilimali zilizopo nchini mwao ni Maudhui ya ndani (Local content) ambayo imelenga sekta ya madini,mafuta na gesi ili kuhakikisha uvunaji katika sekta hizo mbali na kuchangia Pato la Serikali pia linanufaisha watanzania.
Sera hiyo na kanuni zake inalenga kupanua uwanda wa kibiashara kwenye uchumi wa Tanzania,kutengeneza nafasi za ajira kwa kuhamasisha maendeleo ya taaluma na uwezo wa watanzania kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi nchini,
Kwa upande wa sekta ya madini sera hii ya ushirikishwaji Watanzania katika mnyororo wa shughuli za uchimbaji madini Maudhui ya ndani (Local Content) na Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) ambazo zote mbili kwa upande wa sekta ya madini zinasimamiwa na Tume ya Madini chini ya Wizara ya Madini zimeanza kuonyesha mafanikio na kuwa mfano wa kuigwa.
Sheria na sera hizi zikitumika kwenye sekta nyingine zinazoendelea kuvutia wawekezaji kama vile, mawasiliano, fedha,ujenzi , usafirishaji, utalii, na nyinginezo nyingi, Tanzania inaweza kupiga hatua kubwa na kukua kwa kasi kiuchumi na kijamii ndani ya muda mfupi.
Mbali na sera hizo makampuni yaliyowekeza katika sekta ya madini nchini yamekuwa vinara katika kuchangia Pato la Serikali kupitia ulipaji wa kodi ,tozo mbalimbali, kutoa gawio sambamba na kuzalisha ajira nyingi za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja ambazo zimekuwa zikinufaisha Watanzania na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Ukitembelea katika baadhi ya miji iliyo jirani na maeneo ya migodi mikubwa nchini mfano Tarime,Geita,Kahama na sehemu nyinginezo, utaona mabadiliko makubwa ya ukuaji kutokana na uwepo na mzunguko wa fedha kutokana na shughuli za migodi, kuibuka kwa wafanyabiashara wanaotamba katika sekta mbalimbali za biashara ikiwemo usafirishaji pia miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kwa fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) zinazotolewa na makampuni ya madini yaliyowekeza zimefanikisha uwepo wa miundo mbinu bora hususani katika sekta za elimu ,afya, maji na miundombinu ya barabara.
Moja ya kampuni kubwa iliyowekeza katika sekta ya madini nchini ambayo uwekezaji wake unaonekana kuwa wa tija kwa maendeleo ya uchumi wa nchi ni kampuni ya Barrick Mining Corporation ambayo kwa hapa nchini kuanzia mwaka 2019 inaendesha shughuli zake kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals ikiwa inaendesha migodi ya North Mara,Bulyanhulu na Buzwagi ambao uko katika mchakato wa kufungwa.
Akiongea na waandishi wa habari hivi karibuni kuhusu uendeshaji wa shughuli za kampuni nchini,Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow alisema tangu kampuni ianze kuendesha shughuli zake kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga mnamo mwaka 2019 ,imeongeza manunuzi ya bidhaa zake kutoka kwa wazabuni wazawa wa ndani mwaka hadi mwaka hadi kufikia asilimia 83%.
“Tumetekeleza kwa vitendo ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini kwa kufanya manunuzi ya shilingi trillion 1.5 trillioni, ambapo Shilingi trilioni 1.2 (asilimia 75) ilikwenda kwa makampuni ya Watanzania (wazawa) kupitia kanuni ya maudhui ya ndani (local content), na hiyo ni mwaka jana tu,” alisema Bw, Bristow.
Alisema tangu Barrick ichukue usimamizi wa shughuli za madini mwaka 2019, kampuni imewekeza Dola za Kimarekani bilioni 4.79 katika uchumi wa Tanzania, ikiwa ni pamoja na Dola milioni 558 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2025 pekee. Zaidi ya asilimia 90 ya manunuzi yanaendelea kufanywa na wazabuni wa Kitanzania, wengi wao wakiwa makampuni ya kizalendo, na asilimia 96 ya wafanyakazi ni Watanzania, huku asilimia 49 wakitoka katika jamii zinazozunguka migodi hiyo.
Bristow aliongeza kuwa moja ya mfano bora wa utekelezaji wa ushirikiano wa Barrick na Twiga ni mpango wa elimu wa Future Forward, ambao ni uwekezaji wa pamoja wa Dola milioni 30 kati ya Barrick na Serikali, kupitia Ofisi ya Rais, wenye lengo la kupanua miundombinu ya shule kote nchini. Mpango huu uko katika awamu ya pili, na unatarajiwa kutoa nafasi za madarasa kwa wanafunzi zaidi ya 45,000.
Akifungua mkutano wa Jukwaa la 4 la Ushirikishwaji wa Watanzania kwenye sekta ya madini karibuni,Waziri wa Madini Anthony Mavunde alisema sekta ya madini imeweza kuchangia asilimia 9.0% ya Pato la Taifa (GDP) na Serikali mwaka jana imefanikiwa kukusanya maduhuri yenye thamani ya shilingi bilioni 985 , ambayo ni mafanikio makubwa sana.
Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde
Waziri Mavunde alisema katika utekelezaji wa ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini kupitia kanuni ya maudhui ya ndani (Local content) kuna watanzania 16,874 wameajiriwa kwenye sekta ya madini hapa nchini.
Alifafanua zaidi kwamba ni muhimu watanzania ambao ni watoa huduma wazingatie weledi kwenye kazi ya utaoji huduma migodini (compliance) na kujenga utamaduni wa kushirikiana kwa kushikana mikono ili wafanye kazi kwa ufanisi zaidi.
“ndugu zangu watanzania changamkieni hizi fursa kwenye sekta ya madini kwa kushirikiana na serikali itaendelea kutengeneza mazingira mazuri kwa wazawa kuweza kufanya kazi kwenye migodi na kuwajengewa uwezo pamoja na kuhakikisha kwamba taasisi za fedha zinawakopesha,” alisisitiza
Akitoa mada kwenye Jukwaa hilo,Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini kutoka Tume ya Madini nchini , CPA Venance Kasiki, alisema kanuni za ushirikishwaji wa watanzania zilianzishwa mwaka 2018 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2019 na 2023 kutatua matatizo na kero katika ushirkishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini ili kukuza uongezaji wa thamani, kuongeza ajira , kutumia bidhaa na huduma zinazopatikana nchini na kuongeza ushindani wa kimataifa.
“ Serikali iliamua kuja na kanuni ya Maudhui ya Ndani (Local Content) baada ya kilio cha umma (Public Outcry) kuhusu watanzania hususani jamii inayozunguka migodi kutokunufaika na uwepo wa rasilimali madini.Baada ya kilio hicho cha muda mrefu na baadaye kuja kwa sera ya madini ya mwaka 2009 ya kuwawezesha watanzania wazawa kushiriki katika uchimbaji wa madini, kupata kazi za ukandarasi, zabuni na kutoa huduma mbalimbali,” alisema CPA Kasiki.
Aliongeza kwamba fursa za kukuza mnyororo wa thamani kwa watanzania kupitia sekta ya madini ni kubwa na pamoja mambo mengine fursa za kazi kama vile, mitambo ya migodini, Tehama, ujenzi wa viwanda vya kutoa bidhaa kwenye migodi, usafi na ufuaji wa nguo, famasi na tiba na huduma ya chakula.
Â