Feisal Salum maarufu ‘Fei Toto’ ameripotiwa kuwa tayari kusaini mkataba wa kishindo na Simba SC – kwa dau la kuvunja mbavu: bilioni 2! Kwa mujibu wa taarifa zilizoibuka ndani ya kambi ya usajili wa Simba, viongozi wa klabu hiyo wameweka mezani dau la kuvutia ambalo Yanga haikuweza kulingana nalo.
Mo Dewji, bilionea na mfadhili mkuu wa Simba, ndiye anayeaminika kuweka pesa mezani kutimiza ndoto hiyo. Feisal, ambaye alihusishwa kwa muda mrefu kurejea Yanga, sasa anaonekana kupoteza mwelekeo wa kurudi Jangwani – huku Simba wakitumia kila njia kuhakikisha mchezaji huyo mwenye mvuto kwa mashabiki anarudi Ligi Kuu Bara kwa jezi yao.
Kwa mujibu wa chanzo cha ndani, mazungumzo yamefika mbali sana. Feisal anadaiwa kuwa ameridhishwa na mazingira ya Simba, hasa mpango wao wa kumsogeza kwenye soko la kimataifa kupitia CAF Champions League. Aidha, mashabiki wa Simba wamesema wazi kuwa ujio wa Fei Toto unaweza kuimarisha safu ya kiungo ambayo kwa muda mrefu imekuwa na mapungufu.
Kwa upande wa Yanga, juhudi za kumrudisha kiungo huyo ziligonga mwamba baada ya kushindwa kufikia matakwa ya kifedha ya mchezaji huyo. Uongozi wa Yanga haujatoa tamko rasmi, lakini mashabiki wake mitandaoni wameonyesha kukerwa na taarifa hizo huku wakimtaka mchezaji huyo “asiwasaliti”.