
Wakati taifa bado linaomboleza vifo vya wanafunzi sita waliopoteza maisha kwenye ajali ya hivi karibuni huko Chunya, mkoa wa Mbeya umekumbwa tena na msururu wa ajali mbaya ambazo zinasababisha hofu ya vifo zaidi.
Ajali hizo zimeripotiwa kutokea katika maeneo ya mteremko wa Nzovwe kuelekea Daraja la Iyunga jijini Mbeya, eneo ambalo kwa sasa linaendelea na ujenzi wa barabara. Takriban magari matano yameripotiwa kuhusika katika ajali hizo, zikiwemo Coaster mbili za abiria na malori kadhaa.
Katika ajali ya Nzovwe, gari la abiria linalofanya safari kati ya Mbalizi na Nsalaga lilihusishwa na malori mawili, moja likiwa ni la kubeba mchanga. Watu kadhaa wanaripotiwa kujeruhiwa vibaya, huku juhudi za uokoaji zikiendelea kufanywa na vyombo vya usalama pamoja na wananchi.
Wakati huo huo, katika eneo la Iyunga, ajali nyingine imetokea ikihusisha gari aina ya Toyota Coaster lililokuwa likisafirisha abiria kati ya Mbalizi na Stendi Kuu, likigongana na lori lililokuwa na shehena ya saruji pamoja na magari mengine madogo.
Taarifa rasmi kutoka mamlaka husika bado hazijatolewa kuhusu idadi kamili ya vifo au majeruhi, lakini mashuhuda wanasema hali ya majeruhi wengi ni mbaya.
Hali hii inaongeza majonzi kwa wakazi wa Mbeya na taifa kwa ujumla, hasa ikizingatiwa kuwa bado wapo katika maombolezo ya ajali ya Chunya.