MABOSI wa Simba wapo siriazi na ishu za usajili, sema wenyewe mambo yao wanafanya kimyakimya, wakitaka kuja kuwasapraizi mashabiki wa klabu hiyo mara watakapokuwa wakiwatambulisha kwa ajili ya kuanza maandalizi ya msimu mpya wa mashindano kuanzia wiki ijayo.
Inadaiwa kuwa tayari kuna vyuma kadhaa vimeshamalizana na Simba na kilichobaki ni kuweka hadharani na mmoja ya nyota hao wapya ni kiungo Msenegal aliyegeuka gumzo kwa sasa baada ya kutajwa ndiye aliyekuwa akisakwa badala ya Balla Mousa Conte aliyetua Yanga.
Kiungo huyo mpya wa Simba, Allasane Maodo Kanté ameweka wazi kuwa anaiona Tanzania na hasa klabu ya Simba, kama sehemu sahihi ya kuonyesha uwezo wake kwa ukubwa, huku akisisitiza yupo tayari kwa changamoto mpya baada ya kuaga CA Bizertin, Tunisia.
Inadaiwa Kanté atasaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na Wekundu wa Msimbazi kwa ada inayokadiriwa kufikia dola 170,000 za Kimarekani, huku Simba ikikubali pia kuweka kipengele cha asilimia 10 ya mauzo ya baadaye kama sehemu ya makubaliano na CA Bizertin.
Kiungo huyo anatajwa kama mbadala wa kiungo mkabaji kutoka DR Congo, Fabrice Ngoma, ambaye ameachana na klabu hiyo hivi karibuni.
Akizungumza akiwa njiani kurejea Senegal, Kante alisema: “Nimeondoka Tunisia kwa heshima kubwa, lakini sasa ninaangalia maisha mapya. Tanzania ni nchi ninayoiheshimu, lakini zaidi ni klabu ya Simba ni timu kubwa barani Afrika, yenye mashabiki wengi na presha nzuri kwa mchezaji anayetaka kuonesha thamani yake. Naamini huu ndio wakati wangu.”
Kante ambaye ana uzoefu mkubwa wa ligi ya Tunisia, amecheza zaidi ya mechi 80 ndani ya misimu mitatu aliyohudumu CA Bizertin, akionyesha uwezo wa kukaba na kusaidia mashambulizi.
Sifa hizo ndizo zilizomvutia kocha wa Simba, Fadlu Davids, ambaye anaripotiwa kumfuatilia kwa muda mrefu kabla ya kuridhia usajili wake.Alikuwa akiwafuatilia Kante pamoja na Balla Moussa Conte ambaye amejiunga na Yanga akitokea CS Sfaxien ya nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka Simba, Fadlu alizungumza na Kanté binafsi kupitia mtandao, akamweleza kwa kina malengo ya klabu, nafasi anayotarajiwa kupewa kikosini, na namna mfumo wa timu unavyoweza kumfaa kama mchezaji mwenye mtazamo wa kiushindani.
Kabla ya kuwasili Tanzania, Kante atasalia Senegal kwa siku chache akiwa na familia yake, kisha ataanza safari ya kujiunga rasmi na kikosi cha Simba kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya unaotarajiwa kuwa wa ushindani mkubwa.
Kante alisema anajua changamoto ya kucheza katika klabu kubwa kama Simba si jambo dogo, lakini kwa uzoefu wake wa soka Afrika Kaskazini na mazingira yenye presha, haogopi bali anachukulia kama nafasi ya kujijenga zaidi.
“Nilicheza mechi ngumu Tunisia, dhidi ya timu zenye historia, mbele ya mashabiki wengi. Sasa ninaingia Simba nikiwa tayari. Najua kuna mashabiki wenye kiu ya mafanikio, najua kuna malengo makubwa ya timu lakini pia najua nina kitu cha pekee cha kuonyesha Afrika,” alisema.
Kante ameweka wazi kuwa moja ya ndoto zake kubwa ni kuonekana zaidi kwenye michuano mikubwa kama Ligi ya Mabingwa Afrika, jambo ambalo alisema Simba ni sehemu sahihi kwa hilo.
Alisema anapenda kuwa sehemu ya timu yenye ndoto kubwa, na tayari anajua kuwa ushindani wa namba ndani ya Simba ni sehemu ya ukuaji wake binafsi.
Kwa mujibu wa rekodi, Kanté ni mchezaji mwenye umri wa miaka 24, aliyeanzia soka lake nchini kwao Senegal kwa kuzichezea OD Ziguinchor na US Gorée kabla ya kusajiliwa na timu za Kaskazini mwa Afrika.
Anaelezwa kuwa mchezaji mwenye uwezo wa kucheza kama kiungo wa kati wa kukaba (defensive midfielder) na hata namba 8, akitofautiana na Ngoma kwa mtindo wa kiuchezaji unaohusisha kasi na kupandisha mashambulizi.
The post BAADA YA KUMKOSA BALLA CONTE….SIMBA KUSHUSHA ‘SAPRAIZE’ HII..NI MASHINE YA KAZI…. appeared first on Soka La Bongo.